Rais Xi asema China na Russia zimepata njia sahihi ya kutendeana kati ya nchi kubwa jirani (5)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 08, 2025
Rais Xi asema China na Russia zimepata njia sahihi ya kutendeana kati ya nchi kubwa jirani
Rais wa China Xi Jinping akiwasili Moscow, Russia, Mei 7, 2025. (Xinhua/Ding Haitao)

MOSCOW - Rais wa China Xi Jinping juzi Jumanne alitoa hotuba ya maandishi wakati akiwasili Moscow kwa ziara ya kiserikali nchini Russia na kushiriki kwenye sherehe za kuadhimisha miaka 80 tangu kupatikana ushindi katika Vita Vikuu vya Kulinda Nchi vya Umoja wa Kisovieti, ambapo amesema kuwa China na Russia zimepata njia sahihi ya kutendeana kati ya nchi kubwa jirani.

Rais Xi amesema kuwa nchi hizo mbili ni majirani wema wasioweza kuhamishwa, marafiki wa kweli katika dhiki na faraja, na washirika wazuri wa kufanikishana, wameanzisha moyo wa ushirikiano wa kimkakati wa zama mpya, ambao kiini chake ni urafiki na ujirani mwema wa kudumu, uratibu wa kimkakati wa pande zote na ushirikiano wa kunufaishana.

Rais Xi amesema, uhusiano huo wa pande mbili ulio wa kujitawala na kujiamulia unaostahimili magumu, si kama tu unaleta manufaa makubwa kwa watu wa nchi hizo mbili, bali pia unatoa mchango muhimu kwa ajili ya kulinda utulivu wa kimkakati duniani na kuhimiza dunia ya ncha nyingi yenye usawa na utaratibu.

“Mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 80 tangu kupatikana ushindi katika Vita vya Dunia vya Kupambana na Ufashisti na maadhimisho ya miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa,” amesema.

Amesema, China na Russia zikiwa nchi kubwa za dunia na wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, zitashikana mikono kulinda matokeo ya ushindi wa Vita vya Pili vya Dunia, kulinda kithabiti mfumo wa kimataifa ambao kiini chake ni Umoja wa Mataifa na utaratibu wa kimataifa unaowekwa kwenye msingi wa sheria za kimataifa, kupinga kithabiti umwamba na siasa ya mabavu, kufanya ushirikiano wa kweli wa pande nyingi, na kuhimiza ujenzi wa mfumo wenye haki na usawa zaidi wa usimamizi wa dunia.

Rais huyo wa China pia amesema, katika ziara yake hiyo atakuwa na mazungumzo ya kina na Rais Vladimir Putin wa Russia juu ya uhusiano wa pande mbili, ushirikiano wa kufuata hali halisi, na pia kuhusu masuala makubwa ya kimataifa na ya kikanda ya kufuatiliwa kwa pamoja, ili kuingiza nguvu kubwa katika maendeleo ya uhusiano wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati wa pande zote kati ya China na Russia katika zama mpya.

Rais Xi amesema kuwa, atashiriki tena kwenye sherehe za maadhimisho ya Siku ya Ushindi ya Mei 9 ya Russia baada ya muongo mmoja, anatarajia kujiunga pamoja na viongozi wa nchi nyingine na watu wa Russia katika kukumbuka kwa kina wahanga ambao walijitoa kishujaa maisha yao kwa ajili ya ushindi katika Vita vya Dunia vya Kupambana na Ufashisti, na kutoa sauti kubwa ya zama tulizonazo ili kulinda haki na usawa wa kimataifa.

Ndege iliyokuwa imembeba Rais Xi ilisindikizwa na ndege ya Jeshi la Anga la Russia baada ya kuingia katika anga ya nchi hiyo.

Alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Vnukovo mjini Moscow, alikaribishwa kwa furaha na Naibu Waziri Mkuu wa Russia Tatyana Golikova na mafisa wengine waandamizi wa serikali.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha