

Lugha Nyingine
UNESCO latoa wito upya wa kuimarishwa ulinzi wa maeneo ya urithi ya Afrika
![]() |
Picha hii iliyopigwa Aprili 15, 2023, ikionyesha maandhari ya magofu ya Gedi katika Kaunti ya Kilifi, Kenya. (Xinhua/Han Xu) |
NAIROBI - Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limetoa wito tena wa kuimarishwa ulinzi na utambuzi wa maeneo ya urithi ya Afrika, kutokana na mchango wao katika fahari ya kitamaduni na utalii.
Louise Haxthausen, Mkurugenzi wa UNESCO Kanda ya Afrika Mashariki, amesema kwenye mkutano wa kimataifa kuhusu urithi wa kitamaduni barani Afrika Jumanne wiki hii, unaotazamiwa kuhitimisha leo Nairobi, mji mkuu wa Kenya, kwamba bara hilo ni hifadhi ya maeneo maarufu duniani ya kiakiolojia na sanaa za kale za thamani ambavyo vinapaswa kuhifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Haxthausen amesema kuwa sera na mfumokazi mzuri wa kisheria unahitajika ili kuimarisha ulinzi katika maeneo ya urithi ya Afrika huku kukiwa na matishio yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu.
Mbinu jumuishi zaidi unaoshirikisha watunga sera, jumuiya za wenyeji na washirika wa pande nyingi unahitajika ili kuimarisha mjadala wa uelewa kuhusiana na uhifadhi wa maeneo ya urithi katika bara hilo, Haxthausen amesema, akiongeza kuwa Ajenda ya Umoja wa Afrika 2063 inahamasisha kulinda afya ya maeneo na miundombinu ya kihistoria katika bara hilo, kutokana na thamani yao ya kiurithi kwa jamii za wenyeji.
Kwa mujibu wa UNESCO, Afrika inachukua asilimia 12.26 ya Maeneo ya Urithi wa Dunia duniani, lakini mustakabali wa maeneo hayo hauna uhakika kutokana na tishio la ukuaji wa haraka wa miji, sheria dhaifu za ulinzi na shinikizo za tabianchi.
Wahudhuriaji wa mkutano huo ulioanza Mei 6 na utafikia tamati leo Mei 9, ulioitishwa na UNESCO, serikali ya Kenya, na Mfuko wa Urithi wa Dunia wa Afrika, ni pamoja na watunga sera waandamizi, wasomi na wadau wa utamaduni.
Katika kipindi chote cha mkutano huo, wamekuwa wakitafuta namna ya uingiliaji kati wenye kuchochewa na sera, sayansi na jamii unaoweza kuongeza uhimilivu wa maeneo ya urithi ya Afrika.
Waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi wa Kenya Hanna Wendot Cheptumo ametoa wito wa kunufaika pamoja mbinu bora, uhamishaji wa teknolojia na uratibu wa kisera ili kuimarisha ulinzi wa maeneo hayo ya kihistoria barani humo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma