Rais Xi kuhudhuria ufunguzi wa mkutano wa nne wa mawaziri wa Jukwaa kati ya China na CELAC

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 12, 2025

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping atahudhuria na kutoa hotuba kwenye ufunguzi wa mkutano wa nne wa mawaziri wa Jukwaa kati ya China na CELAC (Jumuiya ya Nchi za Latin Amerika na Caribbean) mjini Beijing Mei 13, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China ametangaza jana Jumapili.

Kama ilivyokubaliwa na China na CELAC, mkutano huo utafanyika Beijing Mei 13, na utaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, msemaji huyo ameeleza.

Mawaziri wa mambo ya nje, wajumbe kutoka nchi za CELAC, na wakuu wa mashirika husika ya kikanda watahudhuria mkutano huo, amesema msemaji huyo.

Kwenye mkutano huo na waandishi wa habari jana Jumapili kuhusu mkutano huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China Miao Deyu amesema kuwa Rais Xi Jinping atahudhuria kwenye ufunguzi wa mkutano na kutoa hotuba muhimu, kukumbuka maendeleo ya uhusiano kati ya China-LAC (Latini Amerika na Caribbean), kueleza hali ya uhusiano mzuri, mafanikio, na matarajio mapana ya jumuiya ya China na LAC yenye mustakabali wa pamoja, na kupendekeza mipango na hatua mpya za kuendeleza uhusiano, ambayo itatoa mwongozo na kuingiza hamasa mpya kwa maendeleo tulivu na ya muda mrefu ya uhusiano kati ya China na LAC.

“Mkutano huo unatarajiwa kupitisha nyaraka nyingi za matokeo ya ushirikiano katika maeneo kama vile uvumbuzi wa teknolojia, uwekezaji katika uchumi na biashara, teknolojia ya AI, mambo ya fedha, miundombinu, kilimo na usalama wa chakula, viwanda na teknolojia ya upashanaji habari, nishati na madini, na ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, ikionyesha nia thabiti ya pande zote mbili kwa amani, maendeleo na ushirikiano,” Miao amesema.

Akisema kuwa mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa rasmi kwa Jukwaa hilo kati ya China na CELAC, Miao amesema kufanya mkutano huo wa nne wa mawaziri ni hatua muhimu iliyokubaliwa na pande zote mbili ya kufanyia majumuisho mambo yaliyopita, kujadili ushirikiano na kutafuta mustakabali wa pamoja.

"Kwa umuhimu mkubwa katika ushirikiano kati ya China na LAC, mkutano huo wa nne wa mawaziri utatoa ishara wazi ya China na nchi za CELAC kuitaka dunia kufanya mshikamano na ushirikiano ili kukabiliana pamoja na changamoto zinazoikabili dunia nzima," amesema Miao.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha