Benki Kuu za EAC zakadiria ukuaji wa asilimia 5.8 wa uchumi wa kikanda mwaka 2025

(CRI Online) Mei 12, 2025

Benki Kuu za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimekadiria ukuaji wa uchumi wa kanda hiyo kufikia asilimia 5.8 mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano wa 28 wa Kamati ya Masuala ya Fedha ya EAC, Gavana wa Benki Kuu ya Kenya na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kamau Thugge amesema, mtazamo wa ukuaji utaungwa mkono na maendeleo imara katika sekta za kilimo na huduma.

Mkutano huo ulihudhuriwa na magavana wa Benki Kuu kutoka Burundi, Kenya, Uganda, Tanzania, Somalia, Rwanda na Sudan Kusini.

Magavana hao wamesema, licha ya mtazamo chanya wa ukuaji, hatari bado zipo, hasa kutokana na mvutano wa biashara duniani, wasiwasi wa siasa za kijiografia, na mabadiliko ya tabianchi.

Thugge amesema, ukuaji wa uchumi katika kanda ya Afrika Mashariki umeendela kuwa tulivu licha ya mishtuko ya kimataifa, hasa kutokana na ufanisi imara katika sekta za kilimo, huduma, madini na mafuta.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha