

Lugha Nyingine
China na Marekani zatangaza hatua za kupunguza hali ya wasiwasi ya ushuru
GENEVA - China na Marekani zimetangaza mjini Geneva, Uswisi jana Jumatatu hatua za kurekebisha ushuru zinazolenga kupunguza hali ya wasiwasi ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili zenye uchumi mkubwa zaidi duniani kufuatia mazungumzo ya siku mbili ya ngazi ya juu kuhusu masuala ya kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili.
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa, pande zote mbili zimetambua umuhimu wa uhusiano wao wa kiuchumi na kibiashara kwa nchi zote mbili na uchumi wa dunia, ikisema kuwa pande zote mbili zimesisitiza haja ya kuwepo uhusiano endelevu, wa muda mrefu na wenye kunufaishana wa kiuchumi na kibiashara.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Marekani itasimamisha kutoza asilimia 24 ya ushuru unaolingana na thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini China (pamoja na Mkoa wa Utawala Maalum wa Hong Kong na Mkoa wa Utawala Maalum wa Macau) kwa siku 90 kuanzia Aprili 2, huku ikibakiza kiwango cha asilimia 10 cha ushuru kwa bidhaa hizo. Pia itaondoa ushuru unaoongezeka kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka China unaotangazwa Aprili 8 na 9 mtawalia.
Kwa mujibu wa Amri Tendaji 14259 iliyotolewa Aprili 8 na Ikulu ya White House, Marekani ilipandisha kiwango cha ushuru "wa kutozana kwa usawa" kwa China hadi asilimia 84. Siku moja baadaye, Ikulu ya White House katika amri tendaji nyingine ilipandisha kiwango hicho hadi asilimia 125.
Kwa upade wa China, taarifa hiyo imeeleza kuwa, China itarekebisha ipasavyo matumizi ya kiwango cha ongezeko la ushuru unaotozwa kulingana na thamani ya bidhaa kwa bidhaa za Marekani kama ilivyoainishwa katika Tangazo la Kamisheni ya Ushuru wa Forodha ya Baraza la Serikali la China No. 4 la Mwaka 2025, kwa kusimamisha asilimia 24 ya kiwango hicho kwa muda wa siku 90, huku ikibakiza kiwango cha ushuru huo cha asilimia 10 kwa bidhaa hizo.
Inaeleza kuwa, China itaondoa viwango vya ongezeko la ushuru unaotozwa kulingana na thamani ya bidhaa vilivyorekebishwa kwa bidhaa vilivyowekwa na matangazo No. 5 na No. 6 yaliyotolewa na Kamisheni ya Ushuru wa Forodha ya Baraza la Serikali la China Aprili 9 na 11 mtawalia.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, China pia itachukua hatua zote hitajika za kiutawala kusimamisha au kuondoa hatua zisizo za kiushuru zilizochukuliwa dhidi ya Marekani tangu Aprili 2, 2025.
Taarifa imeeleza kuwa, pande hizo mbili zimeahidi kuchukua hatua kabla ya Mei 14.
Pande hizo mbili pia zimetangaza kuanzisha utaratibu wa kuendeleza mazungumzo kuhusu uhusiano wa kiuchumi na kibiashara ambapo imeelezwa katika taarifa hiyo kuwa mazungumzo hayo yanaweza kufanywa kwa zamu nchini China na Marekani, au nchi ya tatu kwa kukubaliana.
Upandaji mahindi waingia kipindi cha kilele katika Mkoa wa Mongolia ya Ndani, China
UNESCO latoa wito upya wa kuimarishwa ulinzi wa maeneo ya urithi ya Afrika
Maonyesho ya Kimataifa ya Baiskeli ya China 2025 yaanza Shanghai
Shaolin Kungfu, chombo muhimu cha mawasiliano ya Utamaduni wa China na ulimwengu wa nje
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma