

Lugha Nyingine
Uturuki yasema iko tayari kuunga mkono mazungumzo ya amani kati ya Russia na Ukraine
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan (katikati), Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan, Ayman Safadi (kushoto) na waziri wa mambo ya nje wa Syria, Asaad al-Shibani, wakihudhuria mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Ankara, Uturuki, Mei 12, 2025. (Mustafa Kaya/ kupitia Xinhua)
ANKARA - Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky jana Jumatatu, akisisitiza dhamira ya Uturuki katika kuwezesha mazungumzo ya amani kati ya Russia na Ukraine, kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya Erdogan.
Erdogan amesisitiza kuwa usimamishaji vita wa pande zote ni muhimu ili kuweka mazingira mwafaka kwa ajili ya kuanzisha mazungumzo na amehimiza pande zote kutumia fursa ya sasa kwa ajili ya mazungumzo ya kidiplomasia yenye lengo la kumaliza mgogoro huo.
Ameeleza utayari wake wa kuwa mwenyeji wa wajumbe wa Russia na Ukraine nchini Uturuki wakati wa mazungumzo ya amani.
Mazungumzo hayo kwa njia ya simu na Zelensky yamekuja siku moja tu baada ya Erdogan kuzungumza na Rais wa Russia Vladimir Putin, ambapo rais huyo wa Uturuki alisema kuwa nchi yake iko tayari kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani kati ya Russia na Ukraine mjini Istanbul tena.
Akizungumza baada ya mkutano wa baraza la mawaziri siku ya Jumatatu, Erdogan alisema Uturuki imekuwa "mhusika mkuu katika diplomasia ya amani ya kimataifa," akitoa mfano wa jukumu lake katika kutoa upatanishi, misaada ya kibinadamu, na utatuzi wa migogoro.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan ameunga mkono ujumbe huo wa rais, akisema kuwa Uturuki iko "tayari kutoa mchango, haswa katika suala la kuwezesha na kuwa mwenyeji wa" mazungumzo ya amani kati ya Russia na Ukraine.
Kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Ankara na wenzake wa Syria na Jordan, Fidan amesema kuwa majadiliano bado yanaendelea kuhusu muundo wa mazungumzo hayo.
"Ukraine inataka kusimamisha vita kabla ya mazungumzo kuanza, wakati Russia inapendelea kuanza mazungumzo kabla ya makubaliano yoyote ya kusimamisha vita kutangazwa," Fidan amesema, akiongeza pande zote mbili zinatafuta uungwaji mkono unaoendelea wa Marekani.
"Licha ya hayo, msimamo wetu uko wazi. Tunakaribisha pande zote mbili kuja pamoja haraka iwezekanavyo ili kuanzisha usimamishaji vita," amesema.
Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari katika Ikulu ya Kremlin juzi Jumapili, Putin alipendekeza kurejeshwa kwa majadiliano ya upatanishi ya moja kwa moja na Ukraine Mei 15 mjini Istanbul, akisema kwamba Russia inaendelea kuwa na dhamira ya mazungumzo ya makini na Ukraine ili kushughulikia sababu kuu za mgogoro huo unaoendelea na kuweka msingi wa amani ya kudumu na thabiti.
Katika kujibu kauli hiyo ya Rais Putin, Zelensky alisema ni ishara nzuri kwamba Russia imeanza kufikiria kumaliza vita. Hata hivyo, alikuwa amehitaji usimamishaji vita kuanzia jana Jumatatu kama hatua ya kwanza kuelekea lengo.
Mwaka 2022, wapatanishi wa Russia na Ukraine walifanya mazungumzo ya moja kwa moja mjini Istanbul lakini walishindwa kufikia makubaliano juu ya kusimamisha mapigano.
Upandaji mahindi waingia kipindi cha kilele katika Mkoa wa Mongolia ya Ndani, China
UNESCO latoa wito upya wa kuimarishwa ulinzi wa maeneo ya urithi ya Afrika
Maonyesho ya Kimataifa ya Baiskeli ya China 2025 yaanza Shanghai
Shaolin Kungfu, chombo muhimu cha mawasiliano ya Utamaduni wa China na ulimwengu wa nje
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma