Rais wa Iran asema Marekani inaanzisha "vita visivyoisha" kupora rasilimali za nchi nyingine

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 19, 2025

Picha hii ya kumbukumbu inaonyesha Rais wa Iran Masoud Pezeshkian akihudhuria mkutano na waandishi wa habari mjini Tehran, Iran, Septemba 16, 2024. (Xinhua/Shadati)

Picha hii ya kumbukumbu inaonyesha Rais wa Iran Masoud Pezeshkian akihudhuria mkutano na waandishi wa habari mjini Tehran, Iran, Septemba 16, 2024. (Xinhua/Shadati)

TEHRAN - Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema jana mjini Tehran kwamba Marekani imeanzisha "vita visivyoisha" duniani kote ili kupora rasilimali za nchi nyingine na hata nguvukazi za watu, shirika la habari la Iran, IRNA limeripoti.

“Nchi za Magharibi zinajaribu kuzua migogoro katika Mashariki ya Kati ili kumiliki rasilimali za nchi za eneo hilo kwa bei yoyote unayotaka,” Pezeshkian amesema katika ufunguzi wa Baraza la Mazungumzo la Tehran. Mkutano huo wa siku mbili umehudhuriwa na wajumbe 200 wa kigeni, wakiwemo maafisa waandamizi wa serikali na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, kujadili changamoto za kikanda na kimataifa.

Pezeshkian ameongeza kuwa Iran haina cha kuficha na kwa hali yoyote haitasimamisha "mpango wake wa amani wa nyuklia."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Seyed Abbas Araghchi, akizungumza kuhusu mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani- katika hafla hiyo ya ufunguzi, amesema Iran inataka "makubaliano ya haki na yenye uwiano ambayo yataundwa ndani ya mfumokazi wa NPT (Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia) na kwa kuzingatia kuheshimu kikamilifu haki za nyuklia za Iran na kuhakikisha kuondolewa kwa vikwazo kwa njia isiyo ya upendeleo."

"Iran ina dhamira kufanya juhudi za kidiplomasia na inatarajia vikwazo vya upande mmoja, ambavyo vimelenga moja kwa moja watu wetu, vitaondolewa kiukweli na kihalisia," amesema.

Ameongeza kuwa Iran inapenda kufungua ukurasa mpya katika uhusiano kati yake na Ulaya kama Ulaya ina dhamira ya kweli na kuchukua msimamo unaojitegemea kwa Iran.

Wajumbe wa Iran na Marekani wameshafanya raundi nne za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran na kuondolewa kwa vikwazo hivyo vya Marekani katika mji mkuu wa Oman Muscat na Roma ya Italia.

Wakati huo huo, Iran na nchi tatu za Ulaya -- Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, zinazojulikana kwa pamoja kama E3 - zimefanya mkutano wa ngazi ya juu mjini Istanbul Uturuki siku ya Ijumaa juu ya hatua mpya za hivi karibuni katika mazungumzo hayo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, ikiwa ni raundi ya sita ya mazungumzo hayo kati ya Iran na E3 tangu Septemba 2024, ambayo yamekuwa yakiangazia mpango huo wa nyuklia wa Tehran na kuondolewa kwa vikwazo, miongoni mwa masuala mengine.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha