

Lugha Nyingine
China yakaribisha na kuziunga mkono Pakistan na India kushughulikia tofauti kupitia mazungumzo
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akifanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Pakistan ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Mohammad Ishaq Dar mjini Beijing, mji mkuu wa China, Mei 20, 2025. (Xinhua/Zhai Jianlan)
BEIJING - China inakaribisha na kuziunga mkono Pakistan na India kushughulikia ipasavyo tofauti zao kwa njia ya mazungumzo, kufikia usimamishaji vita wa pande zote na wa kudumu na kutafuta suluhu za kimsingi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema jana Jumanne alipokuwa akifanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Mohammad Ishaq Dar.
Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), amesema hayo yanaendana na maslahi ya kimsingi na ya muda mrefu ya pande zote mbili, yanasaidia amani na utulivu wa kikanda, na pia ni matarajio ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa.
"China na Pakistan zimekuwa zikidumisha mawasiliano ya karibu ya kimkakati juu ya kuongeza urafiki wa jadi, kuimarisha ushirikiano wa kunufaishana na kwa pamoja kukabiliana na changamoto, jambo ambalo linaonyesha kiwango cha juu cha uhusiano kati ya pande mbili," Wang amesema.
Ameongeza kuwa, kama marafiki imara kama chuma, China, kama ilivyo wakati wote, itaiunga mkono bila kuyumbayumba Pakistan katika kulinda mamlaka na ukamilifu wa ardhi yake, katika kufuata njia ya maendeleo inayoendana na hali yake ya kitaifa, katika kupambana kithabiti na ugaidi, na kutoa mchango mkubwa zaidi katika masuala ya kimataifa na kikanda.
Wang pia amesisitiza dhamira ya China ya kuzidisha mara kwa mara ushirikiano wa kimkakati wa pande zote wa hali zote na Pakistan.
Ametoa wito kwa pande zote mbili kuungana mkono kujenga awamu mpya ya Ukanda wa Kiuchumi wa China na Pakistan na kuhimiza ushirikiano katika sekta ya viwanda, kilimo, nishati na madini, maendeleo ya rasilimali watu, kukabiliana na ugaidi na usalama.
Kwa upande wake Dar amesema Pakistan inathamini urafiki wa kindugu na China,inashikilia kithabiti kanuni ya kuwepo kwa China moja, na inaunga mkono China katika kulinda maslahi na hadhi yake ya kitaifa.
Ameongeza kuwa Pakistan inafurahia mafanikio mapya ya maendeleo ya China, hasa katika uvumbuzi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, na kwamba inatarajia kuimarisha ushirikiano wa pande zote na China, na inatumai kuendelea kupata uungwaji mkono mkubwa kutoka China katika kuyashinda matatizo ya sasa na kuhimiza maendeleo, usalama na utulivu wa taifa.
Pande hizo mbili pia zimebadilishana maoni kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuzidisha uratibu katika mifumo ya pande nyingi.
Miti ya jacaranda katika mchanuo wa maua yavutia watalii mjini Kunming, China
Upandaji mahindi waingia kipindi cha kilele katika Mkoa wa Mongolia ya Ndani, China
UNESCO latoa wito upya wa kuimarishwa ulinzi wa maeneo ya urithi ya Afrika
Maonyesho ya Kimataifa ya Baiskeli ya China 2025 yaanza Shanghai
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma