Maonyesho ya nne ya uchumi na biashara kati ya China na Afrika kufunguliwa mjini Changsha

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 22, 2025

Watu wakiingia kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano na Maonyesho cha Changsha wakati wa Maonyesho ya tatu ya Uchumi na Biashara ya China na Afrika mjini Changsha, Mkoani Hunan, katikati mwa China, Julai 1, 2023. (Xinhua/Chen Yehua)

Watu wakiingia kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano na Maonyesho cha Changsha wakati wa Maonyesho ya tatu ya Uchumi na Biashara ya China na Afrika mjini Changsha, Mkoani Hunan, katikati mwa China, Julai 1, 2023. (Xinhua/Chen Yehua)

BEIJING - Maonyesho ya nne ya Uchumi na Biashara kati ya China na Afrika yatafanyika Changsha, mji mkuu wa Mkoa wa Hunan katikati mwa China, kuanzia Juni 12 hadi 15, huku watu zaidi ya 12,000 wakitarajiwa kushiriki, waandaaji wa maonyesho hayo wamesema kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana Jumatano.

Maonyesho hayo, yanayoandaliwa kwa pamoja na Wizara ya Biashara ya China na serikali ya mkoa wa Hunan, ni moja ya matukio muhimu zaidi ya uchumi na biashara kati ya China na Afrika mwaka huu ambapo kampuni, jumuiya za wafanyabiashara na taasisi za kifedha zaidi ya 2,800 kutoka China na Afrika zimejiandikisha, pamoja na wawakilishi kutoka nchi 44 za Afrika, mashirika sita ya kimataifa na maeneo 23 ya ngazi ya mikoa ya China.

Yakiwa na kaulimbiu ya "China na Afrika: Kuelekea Mambo ya Kisasa kwa pamoja," maonyesho hayo ya kila baada ya miaka miwili yatajumuisha maonyesho kuhusu sekta zikiwemo za teknolojia na vifaa vya kisasa vya uchimbaji madini, nishati safi, mashine za kisasa za kilimo na vifaa vya ujenzi. Shughuli zaidi ya 20 za kiuchumi na kibiashara zimepangwa kufanyika kwenye maonyesho hayo.

Shen Yumou, mkuu wa idara ya biashara ya mkoa wa Hunan, amesema miradi 128 ya ushirikiano yenye thamani ya jumla zaidi dola bilioni 7 za Kimarekani imetarajiwa kutiwa saini au kukutanisha wadau wakati wa maonyesho hayo, yanayojumuisha maeneo ya viwanda, umeme na nishati, usafirishaji, huduma za upashanaji habari, utamaduni na huduma za afya.

Yakiwa yalizinduliwa mwaka 2019, maonyesho hayo yamepitia hali mbalimbali na kuwa jukwaa kuu la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na Afrika.

Shen Xiang, mkurugenzi wa Idara ya Asia Magharibi na Afrika chini ya Wizara ya Biashara ya China, amesema tukio hilo linatarajiwa kuingiza nishati mpya katika ushirikiano wa kivitendo kati ya pande hizo mbili.

“China imekuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Afrika kwa miaka 16 mfululizo,” amesema Tang Wenhong, naibu waziri wa biashara wa China, akiongeza kuwa mwaka 2024, biashara kati ya China na nchi za Afrika ilifikia rekodi ya juu ya dola za Marekani bilioni 295.6, kiasi ambacho kimeongezeka kwa asilimia 4.8 kuliko mwaka jana wakati kama huo; huku uagizaji bidhaa kutoka Afrika ukifikia dola za Kimaŕekani bilioni 116.8, na kuongezeka kwa asilimia 6.9.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha