

Lugha Nyingine
Balozi wa Somalia nchini China: Hakuna mshirika bora wa ushirikiano kuliko China
Balozi wa Somalia nchini China Dkt. Hodan Osman Abdi amesema, njia ya China ya ujenzi wa mambo ya kisasa si tu inahusisha ujenzi wa miundombinu au ukuaji wa uchumi, bali pia inatafuta maendeleo sambamba na ya pamoja katika uzalishaji mali, kujiamini kiutamaduni na utunzaji wa mazingira.
Akihutubia mkutano wa 14 wa Jukwaa la Majopo ya Washauri Bingwa ya China na Afrika uliofanyika Mei 20 mjini Kunming mkoani Yunnan, Balozi Hodan amesema uzoefu wa China wa kujijenga kuwa nchi ya kisasa unastahili kuigwa na nchi za Afrika, haswa jinsi ya kuweka mipango, kuwekeza katika rasilimali watu na kuendeleza juhudi madhubuti kuelekea lengo la maendeleo ya taifa.
Amesema, katika hali ya sasa ya dunia, Afrika inatakiwa kujiendeleza kupitia kuwezesha watu wake kiuchumi.
Amesema Bara la Afrika lenye watu bilioni 1.4, linaweza kuwa mzalishaji badala ya kuwa mtumiaji tu, na pia linaweza kutoa chakula na nishati endelevu kwa dunia, na kuchochea hamasa ya kufanya ubunifu.
Katika hotuba yake, ameeleza kuwa bara la Afrika, halina mshirika bora wa ushirikiano kuzidi China, kwa kuwa China ina ujuzi, teknolojia na dhamira, na kwamba muhimu zaidi ni kuwa ina uwezo wa kiutendaji wa kuiunga mkono Afrika kufikia malengo yake.
Balozi Hodan amesema, “Katika kumbukumbu ya watu wa kizazi chake, kuna picha isiyoweza kusahaulika ya wahandisi na wafanyakazi wa China wakifanya kazi kwa bidii kuwajengea barabara, madaraja na hospitali.”
Amesema, nchini Somalia barabara pekee ya mwendokasi inayounganisha Kusini na Kaskazini, ilijengwa na China na kwamba chini ya uungaji mkono wa China, Somalia imetekeleza miradi mikubwa zaidi ya 80 ya miundombinu.
Pia ameeleza kuwa, mpunga chotara kutoka China umeisaidia Somalia kuinua kiwango cha kujitosheleza kwa chakula, na kupiga hatua nyingine kuelekea usalama wa chakula.
Balozi Hodan amesema, Somalia ya leo iko katika hatua ya kuingia ukurasa mpya ambapo Mpango wa Mageuzi ya Taifa wa Somalia uliopitishwa hivi karibuni umekusanya mwafaka mpya wa kitaifa, ukiwezesha Somalia kuwekeza katika wananchi wake, kujenga taasisi zenye uhimilivu, na kuendeleza ustawi wa kudumu kwa kutumia faida yake ya kijiografia na mustakbali wa uchumi.
Aidha ameeleza kuwa, Somalia inaungana upya na kanda na dunia, ambapo, mwaka jana ilijiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuwa mwanachama wake wa nane, hatua ambayo imefungua njia mpya kwa Somalia kufanya biashara, uwekezaji na uratibu wa sera, na kuifanya Somalia kuwa kiungo muhimu kinachounganisha Pembe ya Afrika na soko pana la Afrika.
Balozi Hodan amesema, Somalia iko tayari kukaribisha uwekezaji na kuwa mshirika wa ushirikiano wa kimaendeleo na kwamba anatarajia kuwa, katika hatua ijayo, China itajenga viwanda vya utengenezaji bidhaa na vituo vya kuchakata mazao ya kilimo katika nchi za Afrika ikiwemo Somalia.
Amesema, ujenzi wa maeneo maalum ya kichumi, ya viwanda vya kilimo na miundombinu ukiunganishwa na mafunzo ya ufundi stadi, kwa hakika utazisaidia nchi za Afrika ikiwemo Somalia kuzalisha zaidi nafasi za ajira na kuinua uwezo wao wa kukuza uchumi unaoendeshwa na uuzaji nje.
Shughuli za kiutamaduni zafanyika kwenye Jukwaa la Russia na China mjini Khabarovsk, Russia
Miti ya jacaranda katika mchanuo wa maua yavutia watalii mjini Kunming, China
Upandaji mahindi waingia kipindi cha kilele katika Mkoa wa Mongolia ya Ndani, China
UNESCO latoa wito upya wa kuimarishwa ulinzi wa maeneo ya urithi ya Afrika
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma