

Lugha Nyingine
China na Afrika zasherehekea kuimarika kwa uhusiano wao katika Siku ya Afrika mjini Beijing
(Picha/CRI)
Waafrika wanaoishi au kufanya kazi nchini China wameungana na waafrika wenzao duniani kusherehekea Siku ya Afrika ambayo huadhimishwa tarehe 25 Mei ya kila mwaka na kwa mwaka huu imefanyika chini ya kaulimbiu ya "Haki kwa Wafrika na Watu Wenye Asili ya Afrika Kupitia Fidia".
Sherehe hiyo kwa hapa China ilifanyika siku ya Jumamosi mjini Beijing, ikikutanisha mabalozi wa Afrika nchini China, maafisa wa China, wasomi na wawakilishi wa mambo ya utamaduni kujadili mtazamo wa kimataifa kuelekea usawa, ujumuishaji na uelewa wa kihistoria, na kuimarisha urafiki na ushirikiano unaoendelea kukua kati ya China na Afrika.
Akizungumza kwenye sherehe hizo, mwakilishi wa kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) nchini China, Rahmat Allah Mohamed Osman, ametoa shukran zake za dhati akisema China ilikuwa nchi ya kwanza kuunga mkono waziwazi uanachama wa AU katika G20, ikisaidia kupaza sauti ya Afrika katika ngazi ya kimataifa.
Kwa upande wake Martin Mpana, Balozi wa Jamhuri ya Cameroon nchini China ambaye pia ni mkuu wa Umoja wa Mabalozi wa Afrika nchini China, amesisitiza urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika.
Ametilia mkazo kwamba inahitajika dunia iliyo wazi kwa ajili ya watu wote, na si kwa baadhi ya watu kuamulia wengine kutii. Pia ameeleza furaha yake kwamba China na Afrika si tu zinajenga urafiki wa kudumu bali pia ushirikiano wa kunufaishana.
Balozi wa Somalia nchini China, Hodan Osman Abdi, naye ametoa maoni yake kuhusu jinsi maendeleo ya Bara la Afrika yanavyoweza kuendelezwa kupitia uhusiano wake mzuri na Beijing, akisema China imeanzisha jukwaa la ushirikiano wa kunufaishana ambapo maendeleo ya kiuchumi yanajengewa nguvu kwa pamoja.
“China inatoa fursa kwa biashara, kampuni na bidhaa za Afrika kupata masoko yao hapa nchini China” ameeleza.
Wakati huohuo maafisa wa Umoja wa Afrika wamehimiza Waafrika wote kujitolea kujenga Afrika iliyo na umoja, nguvu na ustawi, na yenye uwezo wa kuzungumza kwa sauti moja katika jukwaa la kimataifa.
Wito huo umetolewa kwenye sherehe za Siku ya Afrika katika makao makuu ya AU Jumamosi mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia.
Katika hotuba yake, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Mahmoud Ali Youssouf amesema Afrika inajenga kwa kasi amani, ustawi, na umoja huku ikidai nafasi yake stahiki katika jukwaa la kimataifa.
(Picha/CRI)
Shughuli za kiutamaduni zafanyika kwenye Jukwaa la Russia na China mjini Khabarovsk, Russia
Miti ya jacaranda katika mchanuo wa maua yavutia watalii mjini Kunming, China
Upandaji mahindi waingia kipindi cha kilele katika Mkoa wa Mongolia ya Ndani, China
UNESCO latoa wito upya wa kuimarishwa ulinzi wa maeneo ya urithi ya Afrika
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma