Uganda yasimamisha ushirikiano wa kiulinzi na Ujerumani kutokana na madai ya shughuli za kiuasi za balozi

(CRI Online) Mei 26, 2025

Jeshi la Uganda limesimamisha ushirikiano wote wa mambo ya ulinzi na kijeshi na Ujerumani kutokana na kile kilichoelezwa na msemaji wa jeshi hilo Chris Magezi katika taarifa jana Jumapili kwamba ni ripoti za kuaminika za kijasusi kwamba Balozi wa nchi hiyo nchini Uganda Mathias Schauer anajihusisha kikamilifu na shughuli za uasi nchini humo.

Magezi amesema usimamishaji huo utaendelea kufanya kazi hadi suluhisho kamili litakapopatikana juu ya suala la balozi huyo kujihusisha na vikosi hasimu visivyo halali vya, kijeshi na kisiasa vinavyofanya kazi nchini humo dhidi ya serikali ya Uganda.

Wanasiasa na wafuasi kadhaa wa upinzani wametiwa mbaroni nchini Uganda kutokana na ripoti kuwa wanajihusisha na vitendo vya uasi. Kwa sasa Mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini humo Kizza Besigye anakabiliwa na mashtaka ya uhaini mahakamani.

Mashirika ya usalama yamewaonya wanasiasa wa upinzani kutosababisha machafuko wakati nchi hiyo inapojiandaa kwa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mapema mwaka ujao.

Upinzani umepinga kukamatwa kwa watu hao ukisema wanakabiliwa na mashtaka ya uwongo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha