Waziri wa Mambo ya Nje wa China afanya mazungumzo kwa njia ya simu na wenzake wa Misri na Oman kuhusu mgogoro kati ya Israel na Iran

(CRI Online) Juni 19, 2025

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amefanya mazungumzo kwa njia ya simu jana Jumatano na mwenzake wa Misri, Badr Abdelatty, akisema kitendo cha Israel cha kutozingatia sheria na kanuni za kimataifa kimezidisha ghafla mivutano katika Mashariki ya Kati.

Amesisitiza kuwa China kwa mara nyingine tena inatoa wito kwa pande zote katika mgogoro huo, hasa Israel, kusimamisha mapigano mara moja na kutuliza hali hiyo.

Kwa upande wa jumuiya ya kimataifa, hasa nchi za kikanda Wang amesema katika wakati huu muhimu zinapaswa kujenga zaidi maelewano na kuchukua hatua zaidi katika umoja.

Ameongeza kuwa China iko tayari kushirikiana na Misri ili kuimarisha mawasiliano na uratibu katika majukwaa ya kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa, na kufanya juhudi ya kuhimiza mazungumzo ya amani na maridhiano.

Kwenye mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Sayyid Badr bin Hamad bin Hamood Albusaidi, Wang amesema kuwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran yamekiuka sheria za kimataifa na kanuni zinazosimamia uhusiano wa kimataifa, kukiuka mamlaka na usalama wa Iran, na kudhoofisha amani na utulivu wa kikanda, akibainisha kuwa China imekuwa ikitetea utatuzi wa migogoro yote kwa njia ya amani.

Akisisitiza kwamba kipaumbele cha haraka ni kusimamisha vita na kumaliza mgogoro huo, Wang amesema China inaunga mkono taarifa ya pamoja kuhusu mgogoro huo kati ya Israel na Iran iliyotolewa na nchi 21 za Kiarabu na Kiislamu ikiwemo Oman na inatumai kuwa nchi za Kiarabu na Kiislamu zitaungana na kuendeleza juhudi zao za kusukuma mbele mazungumzo ya amani.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha