Tanzania yatoa wito wa kufanyika utafiti wenye tija kuleta mabadiliko katika sekta ya afya

(CRI Online) Juni 19, 2025

Serikali ya Tanzania imehimiza watafiti na watunga sera kuwekeza katika utafiti wenye tija ili matokeo yake yatumike kutunga sera na mipango itakayoleta mageuzi katika sekta ya afya.

Wito huo umetolewa jana Jumatano na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, katika Kongamano la 13 la Kisayansi lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) linalofanyika kwenye kituo cha magonjwa ya moyo Kampasi ya Mloganzila.

Wito huo umeenda sambamba na wataalamu wa TEHAMA, afya na wasimamizi wa mifumo kuwekeza kwenye matumizi ya teknolojia katika kutoa huduma za afya ili kutambua na kuzuia magonjwa kupitia mifumo hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Daniel Mushi amesema uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali katika chuo hicho unachochewa na matokeo chanya ambayo MUHAS imekuwa ikionesha katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha