Trump asema Marekani itafanya mazungumzo na Iran wiki ijayo

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 26, 2025

Rais Donald Trump wa Marekani (mbele) akihudhuria mkutano na waandishi wa habari kufuatia mkutano wa kilele wa NATO mjini The Hague, Uholanzi, Juni 25, 2025. (Xinhua/Zhao Dingzhe)

Rais Donald Trump wa Marekani (mbele) akihudhuria mkutano na waandishi wa habari kufuatia mkutano wa kilele wa NATO mjini The Hague, Uholanzi, Juni 25, 2025. (Xinhua/Zhao Dingzhe)

THE HAGUE - Rais Donald Trump wa Marekani jana Jumatano kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini The Hague kufuatia mkutano wa kilele wa NATO amesema kuwa Marekani itafanya mazungumzo na Iran wiki ijayo, ambapo amenukuliwa akisema: "Tutazungumza nao wiki ijayo, na Iran. Huenda tukasaini makubaliano".

Mapema siku hiyo ya Jumatano, Trump alisema kwamba usimamishaji vita kati ya Iran na Israel unakwenda "vizuri sana."

"Nadhani (unakwenda) vizuri sana. Israel ilirudi jana," Trump aliwaambia waandishi wa habari kwenye mkutano wa kilele wa NATO mjini The Hague, akirejelea onyo lake la Jumanne kwa Israel kusitisha mashambulizi ya anga dhidi ya Iran.

Juni 13, Israel ilianzisha mashambulizi makubwa ya anga katika maeneo tofauti nchini Iran, yakiwemo maeneo ya nyuklia na ya kijeshi, yakiua makamanda waandamizi, wanasayansi wa nyuklia na raia. Iran ilijibu kwa kurusha duru kadhaa za makombora na droni dhidi ya Israeli, yakisababisha vifo, majeruhi na uharibifu mkubwa.

Siku ya Jumamosi, wiki iliyopita Jeshi la Anga la Marekani lilishambulia kwa mabomu maeneo matatu ya nyuklia ya Iran ya Fordow, Natanz na Isfahan. Katika kulipiza kisasi, Iran Jumatatu wiki hii ilishambulia Kambi ya Jeshi la Anga la Marekani ya Al Udeid nchini Qatar kwa makombora.

Kufuatia shambulizi hilo la Iran, Trump alitangaza kwamba usimamishaji vita kati ya Iran na Israel utaanza majira ya karibia saa 0400 GMT siku ya Jumanne. Pande zote mbili baadaye zilithibitisha kuanza kwa usimamishaji huo wa vita.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha