Beijing yazindua treni ya kwanza ya mizigo kati ya China na Ulaya kuvuka Bahari ya Caspian

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 01, 2025
Beijing yazindua treni ya kwanza ya mizigo kati ya China na Ulaya kuvuka Bahari ya Caspian
Treni ya mizigo ya China-Ulaya ikisubiri kuondoka katika Bandari ya Kimataifa ya Nchi Kavu ya Beijing katika Wilaya ya Fangshan ya Beijing, mji mkuu wa China, Juni 30, 2025. (Xinhua/Zhang Chenlin)

BEIJING - Treni ya mizigo kati ya China na Ulaya imeondoka Beijing, China jana Jumatatu, ikiashiria uzinduzi wa huduma ya kwanza ya usafirishaji mizigo kwa njia mbalimbali ya mji mkuu huo wa China kuvuka Bahari ya Caspian ambapo treni hiyo, ikiwa imepakiwa kontena 104 zilizobeba tani zaidi ya 2,300 za bidhaa kama vile vipuri vya magari, mashine na vitabu, inaelekea Baku, mji mkuu wa Azerbaijan.

Njia hiyo inatumia usafiri wa njia mbalimbali za reli-bahari-reli, inachukua kilomita zaidi ya 8,000 na kupunguza muda wa usafirishaji kutoka siku takriban 50 hadi takriban 15.

Ikiwa imeondoka kutoka katika Wilaya ya Fangshan, lango la kusini-magharibi mwa Beijing, treni hiyo inatoka nje ya mipaka ya China kupitia Bandari ya Horgos, Mkoa unaojiendesha wa Kabila la Wauygur wa Xinjiang, kaskazini-magharibi mwa China, ikipitia Kazakhstan, kuvuka Bahari ya Caspian kwa feri, na kuendelea kwa reli hadi Baku. Baadhi ya mizigo itasambazwa Georgia, Uturuki, Serbia na kwingineko.

Kwa mujibu wa Lu Peng, mkurugenzi wa ofisi ya biashara ya Wilaya ya Fangshan, kuzinduliwa kwa njia hiyo kunaonyesha hatua kubwa katika kupanua njia mbalimbali za huduma za mizigo kati ya China na Ulaya zinazotoka Beijing na kwamba itasaidia kuunda mtandao jumuishi wa usafirishaji wa kimataifa ukichanganya njia za moja kwa moja za ardhini na usafiri wa reli na bahari.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha