Ardhioevu yalinda spishi za ndege kutoka kwenye uwanda hadi mijini

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 03, 2025
Ardhioevu yalinda spishi za ndege kutoka kwenye uwanda hadi mijini
Picha hii iliyopigwa Juni 20, 2025 ikionyesha bata wenye uso mweupe kwenye Kituo cha Ardhioevu cha London jijini London, Uingereza. (Xinhua/Li Ying)

Kama sehemu muhimu ya mfumo ikolojia wa dunia, ardhioevu hutoa mchango mkubwa katika nyanja nyingi zikiwemo ikolojia, mazingira, uchumi na jamii.

Kikijulikana kama pafu la ziada kwa wakazi wa London, Kituo cha Ardhioevu cha London ni paradiso ya ikolojia ya mijini iliyobadilishwa kutoka ardhi isiyotumika ya kiviwanda kwenye kingo za Mto Thames.

Eneo hilo hapo awali lilikuwa hifadhi nne za maji zinazoendeshwa na Kampuni ya Maji ya Thames, ambayo ilikuwa ikisambaza maji ya kunywa kusini-magharibi mwa London. Kituo cha Ardhioevu cha London kilianza kujengwa mwaka 1995 na kilikamilishwa na kufunguliwa kwa umma mwaka 2000.

Watu wanaotembelea kituo hicho wanaweza kuona spishi mbalimbali za ndege walio hatarini kutoweka, na spishi zaidi ya 200 zinazotazamwa na kurekodiwa katika eneo hilo, kikionyesha mapatano kati ya maisha ya mijini na mazingira ya asili.

Mazingira ya kipekee ya kijiografia ya Mkoa wa Xizang wa China hukuza jamii tofauti za viumbe, yakiwa ni maskani ya spishi nyingi adimu. Katika jitihada za kulinda wanyamapori wa uwanda huo, Xizang imeanzisha mfumo wa hifadhi za mazingira ya asili unaozingatia bustani za taifa.

Korongo mwenye shingo nyeusi, spishi iliyo chini ya ulinzi wa daraja la kwanza nchini China, ni korongo pekee anayezaliana na kuishi katika maeneo ya mwinuko wa juu duniani kote. Korongo huyo si tu ni alama ya baraka na uzuri bali pia ni kiungo muhimu katika mnyororo wa ikolojia, akiakisi hali ya ardhi oevu za mwinuko wa juu kupitia desturi yao ya kuishi na uhamaji.

Katika miaka ya hivi karibuni, Mkoa huo wa Xizang umekuwa ukitekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa ikolojia, ikisababisha idadi ya korongo hao wenye shingo nyeusi kuongezeka kila mwaka, na sasa inazidi elfu kumi.

Iwe ni kwenye nyanda za juu za China au katika mji wa Uingereza, kuishi pamoja kwa mapatano kati ya binadamu na mazingira ya asili bado ni matarajio ya pamoja.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha