Sudan Kusini yakanusha kuwa na makubaliano na Marekani ya kupokea raia wa nchi nyingine wanaofukuzwa na Marekani

(CRI Online) Septemba 05, 2025

Sudan Kusini imesema haijaingia makubaliano yoyote ya kupokea raia wa nchi nyingine waliofukuzwa na Marekani.

Akizungumza na wanahabari mjini Juba jana Alhamisi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya nchi hiyo, Apuk Ayuel Mayen, amesema nchi hiyo ilipokea raia saba wa nchi nyingine na raia wa Sudan Kusini Julai 5, kutokana na ushirikiano wa pande mbili na utawala wa Trump.

Amesisitiza kuwa hakuna majadiliano ya kuwahamishia katika nchi hiyo watu hao wanaofukuzwa, na hakuna makubaliano ambayo yametiwa saini kuhusiana na hilo, isipokuwa kulikuwa na mazungumzo ya pande mbili kuhusu kuwahamisha watu hao saba kati ya serikali yake na serikali ya Marekani.

Raia wa nchi nyingine waliohamishiwa nchini Sudan Kusini ni pamoja na wawili kutoka Myanmar, wawili kutoka Cuba, na mmoja kutoka Vietnam, Laos na Mexico, mtawalia.

Aidha, Mayen amesema kuwa raia 23 wa Sudan Kusini ambao awali walifukuzwa Marekani na kurejeshwa nyumbani, tayari wameungana tena na familia zao.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha