

Lugha Nyingine
Algeria yawa mwenyeji wa maonyesho ya 3 ya biashara ya ndani ya Afrika
Maonyesho ya tatu ya Biashara ya Ndani ya Afrika (IATF2025) yamefunguliwa jana Alhamisi mjini Algiers, huku waandaaji wakitarajia mikataba ya biashara na uwekezaji yenye thamani ya hadi dola bilioni 44 za Kimarekani.
Maonyesho hayo ya wiki moja yaliyoandaliwa kwa pamoja na benki ya Exim ya Afrika, Umoja wa Afrika na Sekretarieti ya Eneo la Biashara Huria la Afrika (AfCFTA), yanatarajiwa kufanyika hadi Septemba 10, yakikutanisha washiriki zaidi ya 35,000 na waonyeshaji 2,000 kutoka nchi zaidi ya 75.
Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria, amezindua maonyesho hayo na kutoa wito wa ushirikiano zaidi wa kiuchumi ili kuongeza mchango wa Afrika duniani.
Amesema, licha ya kuwa na asilimia 30 ya maliasili zote duniani na watu bilioni 1.5, Afrika inachangia asilimia 3 tu ya biashara ya kimataifa na inavutia asilimia 6 tu ya uwekezaji wa kimataifa.
Rais Tebboune amesisitiza kuwa upungufu katika miundombinu, nishati, na ufadhili vinazuia ukuaji barani Afrika, akieleza juhudi za Algeria kuhimiza miradi ya ushirikiano kama vile Barabara kuu ya Trans-Sahara, reli mpya inayounganisha Mali na Niger, na ushirikiano kwenye usafiri wa anga, bahari na benki katika bara hilo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma