

Lugha Nyingine
Uwanja wa Olimpiki uliojengwa na China watumika kwa mara ya kwanza kwa mechi ya kufuzu Kombe la Dunia nchini Chad
N'DJAMENA - Ilikuwa Alhamisi asubuhi iliyo angavu, yenye mwanga wa jua nchini Chad, siku ambayo iliahidi zaidi ya mpira wa miguu pekee – ilimaanisha mwanzo wa zama mpya ya michezo ya taifa hilo. Baada ya miaka mingi ya matarajio, Uwanja wa Olimpiki unaong'aa wa Marshal Idriss Deby Itno ulifungua milango yake, ukitoa maskani mapya nzuri kwa soka la Chad.
Miaka zaidi ya mitano baada ya timu ya wahandisi wa China kufika kwa mara ya kwanza katika taifa hilo la Afrika ya Kati, uwanja huo wenye viti 30,000 sasa umesimama juu ya Mandjafa mjini N'Djamena, mji mkuu wa Chad. Ukiwa ni uwanja mkubwa zaidi nchini humo, umekuwa mwenyeji wa mechi yake ya kwanza, mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia kati ya Chad na Ghana.
Ili kusherehekea mechi hiyo ya kwanza ya kihistoria, Rais Mahamat Idriss Deby Itno aligharamia kwa ukarimu gharama zote za tiketi, huku watazamaji wakijaza viti vyote vipya vinavyomeremeta. Saa chache kabla ya mechi hiyo kuanza, watu walimiminika katika jengo hilo la kisasa, msisimko wao ukiwa dhahiri kwa hatimaye kushuhudia uwanja wao wa nyumbani wa taifa wa soka.
Miongoni mwao ni Madjiadjim Yamara, ambaye alisimama kwa mshangao wa mandhari hiyo. "Ni mzuri sana. Ni kama ninaota. Naipongeza China kwa zawadi hii. Sasa vijana wanaweza kuungana, na soka letu litapiga hatua" amesema.
Kwa Mahamat Alamine Abakar, kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Chad, wakati huo ulikuwa wa kipekee sana.
"Tunakuwa wenyeji wa mechi yetu ya kwanza nyumbani. Ni ndoto iliyotimia. Nilipokuwa kocha, nilicheza mechi nne nje ya Chad, na ilikuwa na matokeo mabaya. Leo, shukrani kwa China, tuna uwanja ambao nchi nyingine zinaweza kuutumia." amesema.
Wakati filimbi ya mwamuzi ilipoashiria kuanza, kishindo kutoka kwa mashabiki kilikuwa kisichoweza kuhimilika masikioni.
Black Stars ya Ghana walipata bao dakika ya 17 pale nahodha Jordan Ayew alipofunga bao baada ya kukimbia vizuri na kupiga pasi, lakini Chad wakapambana, na katika dakika ya 89, Celestin Ecua akafunga bao la kusawazisha. Ingawa Chad ilikuwa tayari imeondolewa kwenye mechi za kufuzu, sare hiyo ya 1-1 ilionekana kama ushindi kwa mashabiki wenye furaha tele wa nyumbani.
Nyuma ya pazia, timu ya matengenezo ya Wachina kutoka Kundi la Kampuni za Uhandisi wa Ujenzi la Shaanxi ilihakikisha kila kitu kuanzia mwanga hadi mfumo wa sauti kinakwenda sawa.
Tang Xianfeng, ambaye awali alifanya kazi katika mradi huo kuanzia kwenye usanifu hadi kukamilika, amesema usiku huo ulikuwa hatua muhimu ya yeye mwenyewe.
"Kuona kaka na dada zetu wa Chad wakishangilia kwenye viti, wachezaji wakikimbia kwenye uwanja wa kijani, na mpira ukigonga nyuma ya wavu, tulihisi miaka yetu ya kazi ngumu haikuwa bure," amesema Tang.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma