

Lugha Nyingine
Mwigizaji Mchina Xin Zhilei ashinda Tuzo ya Mwigizaji Bora kwenye Tamasha la Filamu la 82 la Venice (5)
VENICE, Italia - Mwigizaji Mchina Xin Zhilei ameshinda tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike juzi Jumamosi usiku kwenye Tamasha la 82 la Kimataifa la Filamu la Venice kwa uigizaji wake wa kuhuzunisha katika filamu ya "The Sun Rises on Us All", ambapo ikiwa iliongozwa na mtayarishaji filamu wa China Cai Shangjun, filamu hiyo, inayojulikana kwa Kichina kwa jina la Ri Gua Zhong Tian, inaonyesha mapenzi ya kuhuzunisha ya wapenzi wa zamani yaliyotekwa na hatma na hayakuweza kufikiwa.
Xin alikabidhiwa tuzo hiyo na mwigizaji wa China Zhao Tao, mjumbe wa majaji wa kimataifa wa shindano hilo la mwaka huu.
Katika hotuba yake ya kukubali tuzo hiyo, Xin amesema amehisi heshima na fahari kusimama kwenye jukwaa la tamasha hilo akiwa mwigizaji Mchina.
Amelishukuru kundi la watengenezaji wa filamu hiyo na kutoa maneno ya kutia moyo kwa mabinti wadogo: "Kwa mabinti wote, kama una ndoto, thubutu kuiwazia na kuiendea -- huwezi kujua, inaweza kutimia."
Tamasha hilo la 82 la Kimataifa la Filamu la Venice lilianza Agosti 27 na kufikia tamati Septemba 6 katika kisiwa cha Lido cha mji huo wa Italia, likiwa na filamu 21 katika safu kuu ya mashindano.
Filamu ya mwongozaji wa Marekani Jim Jarmusch ya "Father Mother Sister Brother" imeshinda Golden Lion kwa Filamu Bora. Ilikuwa ni usiku wa "bingwa ambaye hatabiriki," limeandika jarida la burudani la Marekani The Hollywood Reporter.
Ikiwa imegawanywa katika sehemu tatu, filamu hiyo inasimulia simulizi ya ndugu kadhaa na safari zao kwa wazazi wao, ikionyesha uhusiano wa kifamilia.
Wakati akipokea tuzo yake, Jarmusch amesema, "Sisi sote hapa tunaotengeneza filamu, hatuchochewi na ushindani, lakini ninathamini sana heshima hii isiyotarajiwa."
Filamu ya mwongozaji filamu wa Tunisia Kaouter Ben Hania ya "The Voice of Hind Rajab," filamu kuhusu msichana wa Kipalestina aliyeuawa katika mgogoro wa Gaza, imechukua Tuzo Kuu ya Majaji.
Likiwa lilianzishwa mwaka 1932 Tamasha la Filamu la Kimataifa la Venice ni moja ya matamasha ya filamu "Makubwa Matatu" ya Ulaya pamoja na Tamasha la Filamu la Cannes nchini Ufaransa na Tamasha la Kimataifa la Filamu la Berlin nchini Ujerumani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma