

Lugha Nyingine
China yafanya maonyesho ya kimataifa ili kuongeza uwekezaji na biashara (2)
XIAMEN - Maonyesho ya 25 ya Kimataifa ya Uwekezaji na Biashara ya China (CIFIT) yamefunguliwa jana Jumatatu katika mji wa Xiamen, Mkoa wa Fujian, kusini mashariki mwa China, yakivutia wageni kutoka nchi na maeneo zaidi ya 120.
Yakijikita katika maeneo makuu matatu -- "Wekeza nchini China," "uwekezaji wa China" na "uwekezaji wa kimataifa" – maonyesho hayo ya siku nne yanajumuisha zaidi ya shughuli 100 zenye mada za uwekezaji na yanashirikisha Uingereza kama nchi mgeni wa heshima.
Banda la Taifa la Uingereza lenye ukubwa wa mita za mraba 400, likiwa na kaulimbiu ya "Wekeza katika UKUBWA (Invest in GREAT)," linaangazia sekta muhimu kama vile huduma za mambo ya fedha na kitaaluma, viwanda vya hali ya juu, sayansi ya maisha, nishati safi na tasnia za ubunifu.
Lewis Neal, Kamishna wa Biashara wa Uingereza nchini China, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba Uingereza imetuma ujumbe wake mkubwa zaidi wa wafanyabiashara kwenye maonyesho hayo, unaojumuisha kampuni zaidi ya 100 kutoka kote nchini.
Neal ameongeza kuwa wameona CIFIT kama fursa kuu kwa Uingereza kutangaza sekta zinazochochea ukuaji, kama ilivyoainishwa katika mkakati wa kisasa wa viwanda wa nchi hiyo.
Akielezea imani yake katika mtazamo wa uchumi wa China, amesema, "China ni nchi ya pili kwa ukubwa wa uchumi wake duniani na inatarajiwa kukua kwa nguvu. Tuna matumaini kuhusu uwezo kwa kampuni za Uingereza kuja na kukua nchini China."
Maonyesho hayo ya mwaka huu yatafanya kongamano na kampuni za kimataifa, midahalo kati ya kampuni kubwa za kibinafsi na kampuni Bora 500 duniani, na shughuli zaidi ya 30 za kutangaza uwekezaji maalum, zikiwasilisha uhai na fursa za "kuwekeza nchini China" kwa namna pana na ya pande nyingi.
Ujumbe wa kampuni 50 kutoka Shirikisho la Wafanyabiashara wa Marekani Kusini mwa China (AmCham South China) uko kwenye maonyesho hayo ya mwaka huu.
"Kampuni nyingi ni kampuni kubwa za kimataifa, zinazohusika na dawa, vitu vya kutunza mwili na bidhaa za wanunuzi. Kampuni zetu zina nia kubwa ya kutafuta fursa mpya, "amesema Harley Seyedin, mwenyekiti na rais wa AmCham Kusini mwa China, akiongeza kuwa shirikisho hilo limekuwa likiwa na wastani wa dola za Kimarekani zaidi ya bilioni 2 katika mikataba mipya iliyosainiwa kwenye maonyesho hayo kila mwaka katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.
Kwa mujibu wa Seyedin, China inabaki kuwa sehemu yenye kuvutia kwa uwekezaji.
Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Biashara ya China zinaonyesha kuwa kuanzia Januari hadi Juni 2025, kampuni mpya 30,014 zilizowekezwa kwa mtaji kutoka nje zilianzishwa nchini China, ikiwa ni ongezeko la asilimia 11.7 kuliko mwaka jana. Miongoni mwao, matumizi halisi ya mtaji wa kigeni katika viwanda vya teknolojia ya hali ya juu yalifikia yuan bilioni 127.87.
Yakiwa yalizinduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1997, Maonyesho hayo, yanayoandaliwa na Wizara ya Biashara ya China, yamekuwa jukwaa muhimu la kuongeza uwekezaji na kuwezesha maendeleo ya kimataifa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma