

Lugha Nyingine
Viongozi wa Afrika watoa wito wa kuimarishwa kwa masuluhisho ya tabianchi katika Mkutano wa 2 wa Kilele wa Tabianchi wa Afrika
ADDIS ABABA - Viongozi wa Afrika katika Mkutano wa Pili wa Kilele wa Tabianchi wa Afrika jana Jumatatu wametoa wito wa kuchukua hatua kali zaidi za tabianchi na ushirikiano ili kusukuma mbele malengo ya maendeleo ya kijani ya bara hilo.
Ukiwa umeandaliwa na Ethiopia na Umoja wa Afrika (AU), mkutano huo muhimu wa tabianchi barani Afrika unafanyika kuanzia Jumatatu hadi Jumatano mjini Addis Ababa, ukiwakutanisha wakuu wa nchi, mawaziri, wanadiplomasia, washirika wa kimataifa chini ya kaulimbiu ya “Kuharakisha Masuluhisho ya Kimataifa ya Tabianchi: Ufadhili kwa Uhimilivu wa Afrika na Maendeleo ya Kijani."
Akihutubia mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Mahmoud Ali Youssouf amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha "haki na usawa" katika ufadhili wa tabianchi duniani.
Amesema udhaifu wa nchi wanachama wa AU, unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, mzigo wa madeni, na kukosekana usawa kimuundo kwa mfumo wa mambo ya fedha wa kimataifa, lazima vishughulikiwe kupitia haki ya tabianchi.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesisitiza ni lazima kuimarisha ushirikiano wa nchi za bara hilo na hatua za pamoja ili kufikia malengo ya pamoja ya tabianchi.
"Afrika lazima isimame si kama kambi ya wapatanishi, lakini kama bara lenye masuluhisho, kutimiza maono ya Ajenda 2063 kwa mustakabali wenye ustawi, himilivu na vumbuzi. Ni lazima tuifanye Afrika kuwa mahali ambapo dunia inaona malengo ya tabianchi yakifikiwa, ambapo upandaji miti si mradi wa majaribio bali utamaduni, na ambapo kilimo cha kisasa cha tabianchi kinalisha mamilioni ya watu," amesema.
Akiunga mkono maoni hayo, Rais wa Kenya William Ruto ameangazia maendeleo ya Afrika tangu Azimio la Nairobi, ambalo lilipitishwa wakati wa Mkutano wa kwanza wa Kilele wa Hatua za Tabianchi wa Afrika ambao ulifanyika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi mwaka 2023.
"Miaka miwili baadaye, tumepata maendeleo makubwa. Uwezo wetu unatambulika, sauti yetu inasikika, na masuluhisho yetu yanatumika, kuanzia miundombinu ya kijani na kilimo cha kisasa cha tabianchi hadi urejeshaji mazingira, usimamizi wa taka na hata teknolojia mpya za kisasa. Katika bara zima, wajasiriamali na jamii za Afrika zinavumbua na kujenga uhimilivu kutoka chini kwenda juu," amesema.
Mkutano huo unatarajiwa kutoa matokeo makubwa kadhaa, ikiwemo kupitishwa kwa Azimio la Addis Ababa, ambalo litatoa sauti ya pamoja ya Afrika kabla ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) wa 2025 nchini Brazil na kwingineko.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma