Ethiopia yazindua bwawa kubwa zaidi la kuzalisha umeme kwa maji barani Afrika (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 10, 2025
Ethiopia yazindua bwawa kubwa zaidi la kuzalisha umeme kwa maji barani Afrika
Picha iliyopigwa Septemba 9, 2025, ikionyesha Bwawa la Kuzalisha Umeme kwa Maji la Grand Ethiopian Renaissance (GERD) katika eneo la kaskazini-magharibi la Benishangul-Gumuz, Ethiopia. (Xinhua/Michael Tewelde)

ADDIS ABABA – Ethiopia imezindua rasmi Bwawa la Kuzalisha Umeme kwa Maji la Grand Ethiopian Renaissance (GERD), mradi mkubwa zaidi wa kuzalisha umeme kwa maji barani Afrika.

Hafla iliyohudhuriwa na maafisa waandamizi wa Ethiopia, viongozi wa Afrika, wawakilishi kutoka Umoja wa Afrika na mashirika mengine ya kimataifa, wakiwemo Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Mahmoud Ali Youssouf, Rais William Ruto wa Kenya, Rais Ismail Omar Guelleh wa Djibouti na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, imefanyika jana Jumanne karibu na Bwawa hilo katika eneo la kaskazini-magharibi la Benishangul-Gumuz ili kusherehekea kukamilika rasmi kwa mradi huo.

Ujenzi wa mradi huo wa kuzalisha umeme wenye uwezo wa megawati 5,150 ulianza mwaka 2011 kwenye Mto Blue Nile karibu na mpaka na Sudan.

Akihutubia hafla hiyo, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amezungumzia uwezo mkubwa wa bwawa hilo kuimarisha uchumi wa taifa kwa kutoa nishati tulivu kwa viwanda, kuboresha maisha na kusukuma mbele mafungamano ya nishati ya kikanda.

"Hongera kwa Waethiopia wote, kote ndani na nje ya nchi, vilevile marafiki zetu kote duniani, kwa uzinduzi wa kihistoria wa Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance." amesema.

Mradi huo, uliosanifiwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi maji jumla ya mita za ujazo bilioni 74, kwa muda mrefu umekuwa chanzo cha mvutano kati ya nchi tatu ambako mto Nile unapita za Ethiopia, Misri na Sudan. Wakati Misri na Sudan zikihofia bwawa hilo litapunguza kiwango chao cha maji, Ethiopia inashikilia kuwa mradi huo hautazidhuru nchi za sehemu ya mtiririko wa chini wa mto.

"Sisi ni waumini thabiti katika upigaji hatua wa pamoja." Abiy amesema, akisisitiza tena dhamira ya Ethiopia katika kutafuta ukuaji bila kuathiri maslahi ya majirani zake.

Mto Blue Nile, unaojulikana kwa jina la Mto Abay nchini Ethiopia, unaanzia Ziwa Tana umbali wa kilomita karibu 570 kaskazini mwa Addis Ababa na ni moja kati ya mito miwili mikuu ya Mto Nile.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha