

Lugha Nyingine
Maonyesho ya biashara ya huduma ya China yavutia ushiriki wa kimataifa, yaangazia masoko wazi
BEIJING – Yakifanyika katika mabaki ya viwanda yaliyobadilishwa matumizi ya Eneo Maalum la Viwanda la Shougang magharibi mwa Beijing, mji mkuu wa China, Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Huduma ya China 2025 (CIFTIS) yamefunguliwa Jumatano wiki hii, yakiwa na wito wa masoko wazi na uvumbuzi wa kidijitali.
Mwaka huu ni mara ya kwanza kwa maonyesho hayo kufanyika katika eneo hilo la Shougang, eneo la urithi wa kiviwanda lenye ukubwa wa kilomita 3 za mraba na ukumbi wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing 2022. Kaulimbiu yake, "Kumbatia Teknolojia ya kisasa, Wezesha Biashara ya Huduma," inasisitiza lengo ambalo linatoa athari mbali zaidi ya mipaka ya China.
Kiwango cha maonyesho hayo ya mwaka huu ni kikubwa, huku nchi na mashirika ya kimataifa 85 – zikiwemo Australia, Ujerumani na Shirika la Haki Miliki Duniani-- zikishiriki. Kampuni takriban 2,000 zinaonyesha bidhaa ukumbini, zikiwemo kampuni karibu 500 za Kampuni Bora 500 Duniani na kampuni ongozi katika huduma kama vile Walmart, AstraZeneca na KPMG. Washiriki wa maonyesho hayo, haswa, wanatoka nchi 26 kati ya nchi na maeneo 30 bora duniani katika masuala ya biashara ya huduma.
Mageuzi ya uchumi duniani, ambapo huduma sasa ndiyo uti wa mgongo wa ukuaji wa uchumi, yamechukua nafasi kubwa katika hotuba na majadiliano kwenye Mkutano wa Kilele wa Biashara ya Huduma Duniani, ulioandaliwa kwa pamoja juzi Jumatano na Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Biashara na Maendeleo (UNCTAD), Wizara ya Biashara ya China na serikali ya mji wa Beijing.
"Huduma si mshiriki muungaji mkono tena katika biashara ya kimataifa. Ni msukumo wa ukuaji," amesema Johanna Hill, naibu mkurugenzi mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO).
Amesisitiza kuwa sekta hiyo inachukua theluthi mbili ya uchumi wa dunia, nusu ya ajira duniani kote na asilimia 40 ya biashara katika ongezeko la thamani.
China imetumia jukwaa hilo kusisitiza tena ahadi yake ya kufungua mlango. Katika hotuba yake kuu, Naibu Waziri Mkuu wa China Ding Xuexiang alisema kuwa kiwango cha biashara ya huduma nchini humo "kilipata mafanikio mapya mwaka 2024, kikizidi dola trilioni 1 za Marekani kwa mara ya kwanza."
Amehusisha mafanikio hayo na ufunguaji mlango wa kitaasisi wa China wa sekta ya huduma zake, ikiwemo kuanzishwa kwa orodha hasi ya biashara ya huduma ya kuvuka mipaka kote nchini, kupanua ufikiaji wa soko katika mawasiliano ya simu na huduma za afya, kuwezesha biashara ya huduma na sera za msamaha wa visa.
Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa jumla ya thamani ya biashara ya huduma za China ilipanda kwa asilimia 8 kuliko mwaka jana wakati kama huo na kufikia yuan trilioni 3.9 (dola za kimarekani kama bilioni 548.82) katika nusu ya kwanza ya 2025 -- ikifikia rekodi ya kihistoria.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma