Kituo cha Uvumbuzi na Ujasiriamali cha Vijana cha Qianhai Shenzhen-Hong Kong chawa chachu ya maendeleo bora ya hali ya juu duniani (5)

By Aris (Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 16, 2025
Kituo cha Uvumbuzi na Ujasiriamali cha Vijana cha Qianhai Shenzhen-Hong Kong chawa chachu ya maendeleo bora ya hali ya juu duniani
Waandishi wa habari wakitazama vifaa vya urembo wa wanawake kwenye kampuni iliyo katika Kituo cha Uvumbuzi na Ujasiriamali cha Vijana cha Qianhai Shenzhen-Hong Kong, Septemba 15, 2025, (Picha/People’s Daily Online)

Kituo cha Uvumbuzi na Ujasiriamali cha Vijana cha Qianhai Shenzhen-Hong Kong (Ehub) kilichoko Qianhai, mjini Shenzhen, mkoa wa Guangdong, kusini mwa China kimekuwa chachu kubwa ya kusukuma mbele maendeleo bora ya hali ya juu ya China na duniani kote tangu kuanzishwa kwake Mwaka 2014.

Kikiwa ni maskani ya kampuni mbalimbali vumbuzi za teknolojia ya hali ya juu na mahiri za kisasa, kituo hicho kimejikita hasa katika sekta za kimkakati zikiwemo za akili mnemba (AI), roboti changamani za muundo wa binadamu, teknolojia za maisha na afya, teknolojia za kitamaduni na kimichezo na zile za mambo ya fedha.

Kampuni mbalimbali za teknolojia hizo ibuka duniani kama vile Spaceship, Bytelumio, GEE.D, Deep Harbour, i2Cool, Dynamo semiconductor, Lumen Labs, Remo, RiVAI na nyingine nyingi zimeanzia, kuendelea na kuweka makao makuu yao kwenye kituo hicho, zikitumika kama daraja la kusukuma maendeleo bora ya hali ya juu ya China na kuchangia uvumbuzi wa thamani duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari wa China na wa kigeni wa timu ya kufanya utafiti kuhusu Mji wa Shenzhen ya People's Daily Online waliotembelea kampuni ya i2 Cool, moja ya kampuni zilizo kwenye kituo hicho, ofisa mwelekezi katika kampuni hiyo ameeleza kuwa, kampuni hiyo imekuwa ikijikita katika kuvumbua na kuzalisha teknolojia ambazo zinaleta suluhisho kwa ajili ya maendeleo bora ya hali ya juu.

Amesema, kampuni hiyo inajikita hasa katika kutoa suluhisho za kivumbuzi na endelevu za upozaji joto kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ulio rafiki kwa mazingira, matumizi ya viwandani na ulinzi wa afya ya binadamu kwa nchi zaidi ya 35 duniani.

Ameeleza kuwa kampuni hiyo, inaendelea kuunda na kuendeleza teknolojia mpya za hali ya juu za kuhifadhi na kupunguza matumizi ya nishati duniani ili kuunga mkono miji yenye kutoa kaboni chache na jumuiya za kijani duniani kote.

Nyaraka zilizotolewa na kampuni hiyo zinaonesha kuwa, kampuni inazalisha nyenzo za koti la kukinga au kupunguza athari za joto katika majengo kama vile ya makazi, majengo ya maduka, viwanda, karakana, vituo vya data, majengo ya umma. Zinaeleza kuwa, ufanisi wa matumizi ya nyenzo zake ni wenye kupunguza joto la uso wa dunia kwa hadi digrii 42.9 na uhifadhi wa nishati kwa mifumo ya kiyoyozi kwa hadi asilimia 42.

Kituo cha Ehub, ambacho ni sehemu ya mkakati mpana wa China katika kufungamanisha kimaendeleo maeneo ya Guangdong na Hong Kong, hutoa uungaji mkono kwa kampuni zinazoanzishwa hapo katika uwekezaji wa mitaji, uungaji mkono wa kisera, ubia na vyuo vikuu, jumuiya za vijana, ufikiaji masoko ya kimataifa, huduma za kitaalam za kisheria, uendeshaji na menejimenti, makaazi na uendelezaji vipaji na mambo mengine.

Kimejengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 100,000 kikiwa kimesheheni ofisi na vituo vya utafiti na uvumbuzi (R&D) vya kampuni mbalimbali.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha