Lugha Nyingine
Uganda yaingiza mbuzi chotara wa China kuongeza uzalishaji (2)
KAMPALA - Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) nchini Uganda limekabidhi rasmi mbuzi tisa chotara wa China, wanaojulikana pia kwa jina la mbuzi Jianzhou wenye masikio makubwa, kwa taasisi mbili za utafiti za kienyeji ili kuboresha uzao wa mbuzi na kuongeza uzalishaji katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Mbuzi hao -- madume matatu na majike sita -- wamekuwa chini ya karantini tangu Julai baada ya kuingizwa nchini humo kupitia mradi wa Ushirikiano wa Kusini na Kusini (SSC) wa FAO-China-Uganda. Siku ya Alhamisi, walikabidhiwa kwa Shirika la Taifa la Utafiti wa Kilimo la Uganda (NARO) na Kituo cha Taifa cha Rasilimali za Jeni za Wanyama na Benki ya Data kwa ajili ya uzalianaji na utafiti.
Bright Rwamirama, waziri wa Uganda anayeshughulikia sekta ya wanyama, amesema mpango huo ni mwanzo wa juhudi za kupanua uzalishaji wa mbuzi kwa ajili ya kuuza nje ya nchi.
"Madhumuni ya kupata mbuzi hawa ni kwa ajili ya utafiti, kuzaliana na kuwafanya kuwa wengi kwa ajili ya kufikiwa kwa wafugaji," Rwamirama amesema, akiipongeza China kwa kutoa mbuzi hao katika hafla ya kukabidhi mjini Entebbe.
Zhang Xiaoqiang, mkuu wa timu ya kilimo ya China chini ya mradi wa SSC, amesema mbuzi hao wanaonyesha ushirikiano mkubwa wa kilimo kati ya nchi hizo mbili.
"Aina hii ya mbuzi, ninaamini sana, inaweza kutoa mchango katika kuboresha sifa na uzalishaji wa mbuzi nchini Uganda," Zhang amesema.
Mwakilishi wa FAO nchini Uganda Yergalem Taages Beraki amesema kuletwa kwa mbuzi hao wa Jianzhou nchini Uganda ni hatua muhimu katika ushirikiano wa Kusini na Kusini.
Ameongeza kuwa kuzaliana kwa kuchangamana na mbuzi wa kienyeji kutaongeza tija na uhimilivu, ikiongeza mapato, kuboresha lishe, na kuongeza uwezo wa kukabiliana na mishtuko ya tabianchi na soko.
Kwa mujibu wa NARO, mifugo ya asili ya Uganda, kama vile mbuzi wa Mubende na wale Wadogo wa Afrika Mashariki, kwa kawaida huongezeka kilo 25-35 katika miaka miwili, wakati aina hiyo ya Jianzhou inaweza kufikia kilo 45 katika miezi 18.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




