

Lugha Nyingine
Rais wa Misri asema Misri itatoa misaada kwa Gaza baada ya kusimamisha mapigano
CAIRO - Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri amesema kuwa Misri imeanza kutuma msaada wa dharura wa chakula na matibabu katika Ukanda wa Gaza kufuatia Israel na Hamas kufikia makubaliano ya kusimamisha mapigano.
Sisi alitoa kauli hiyo Ijumaa katika mazungumzo kwa njia ya simu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, akisisitiza haja ya kutekeleza kikamilifu makubaliano hayo ya kusimamisha vita, imesema ikulu ya Misri.
Amesisitiza tena uungaji mkono wa Misri kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayofanya kazi Gaza, hasa Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada na Kazi kwa Wakimbizi wa Palestina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA), na kwa juhudi za kusaidia wakimbizi wa Palestina katika nchi zinazowahifadhi.
Kwa upande wake Guterres amesema njia ya kusonga mbele lazima ijumuishe kuundwa kwa Nchi ya Palestina chini ya maazimio ya kimataifa na umoja wa Gaza na Ukingo wa Magharibi. Pia ametoa wito wa kutumwa kwa vikosi vya kimataifa huko Gaza na kuunga mkono Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa makubaliano hayo ya kusimamisha mapigano.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza haja ya dharura ya kuanza ujenzi upya wa Gaza na amekaribisha mkutano wa kimataifa ambao Misri inapanga kuandaa kwa ajili hiyo.
Israel na Hamas walifikia makubaliano ya kusimamisha mapigano siku ya Alhamisi wiki iliyopita baada ya siku tatu za mazungumzo yaliyopatanishwa na Misri, Qatar, Uturuki na Marekani.
Kipindi cha kwanza cha makubaliano hayo kinajumuisha kuondoa wanajeshi wa Israel kutoka Mji wa Gaza, Rafah, Khan Younis na kaskazini, kufunguliwa kwa vivuko vitano vya mpakani kwa ajili ya misaada, na kuachiliwa huru kwa mateka na wafungwa.
Chanzo cha habari ndani ya Hamas kimesema kivuko cha Rafah kati ya Gaza na Misri kinatarajiwa kufunguliwa tena katikati ya wiki hii ili kuruhusu watu wachache kwenda na kurudi, ingawa maelezo zaidi hayajatangazwa.
Operesheni za kijeshi za Israel ambazo zimeendelea zaidi ya miaka miwili zimeiharibu Gaza, zikiua watu zaidi ya 67,000 na kusababisha baa la njaa, takwimu za mamlaka za afya za Gaza zinaonesha.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma