

Lugha Nyingine
Mkutano wa Viongozi Duniani kuhusu Wanawake wamalizika Beijing
BEIJING - Mkutano wa Viongozi Duniani kuhusu Wanawake umefungwa rasmi mjini Beijing Jumatatu alasiri, ambapo Mjumbe wa Serikali ya China ambaye pia ni Mkuu wa Shirikisho Kuu la Wanawake la China Shen Yiqin na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN Women) Sima Bahous wamehudhuria na kutoa hotuba kwenye mkutano huo.
Shen amesema kuwa hatua tano za kivitendo zilizotangazwa na China kwa kuunga mkono maendeleo ya wanawake duniani zimeonyesha uwajibikaji wa nchi hiyo kubwa, na kusifiwa na watu wengi wanaohudhuria mkutano huo na kuitikiwa nao.
"China inapenda kushirikiana na nchi nyingine kubadilisha mapendekezo na maoni ya pamoja yaliyofikiwa katika mkutano huo kuwa hatua za vitendo halisi, ili kusaidia wanawake wengi zaidi kutimiza ndoto zao na kupata mafanikio," ameongeza.
Kwa upande wake Bahous amesifu mafanikio dhahiri yaliyopatikana nchini China katika kusukuma mbele maendeleo ya wanawake na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya wanawake duniani kote, na amehimiza nchi nyingine kuiga uzoefu wenye thamani wa China katika uwanja huo.
Wajumbe wapatao 800 kutoka nchi na mashirika ya kimataifa zaidi ya 110 walihudhuria hafla ya kufungwa kwa mkutano huo, huku taarifa ya mwenyekiti ikitolewa.
Viongozi na wawakilishi kutoka nchi na mashirika ya kimataifa 46 walichangia mawazo yao wakati wa kikao cha wajumbe wote kilichofanyika kabla ya kufungwa kwa mkutano huo, wakiuelezea mkutano huo kuwa ni mnara mpya katika historia ya harakati za wanawake wa kimataifa na kuahidi kuchukua hatua za vitendo halisi ili kuharakisha maendeleo ya wanawake ya pande zote.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma