Misri yafunga Jumba la Makumbusho Kuu la Misri kwa ajili ya kufunguliwa rasmi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 15, 2025
Misri yafunga Jumba la Makumbusho Kuu la Misri kwa ajili ya kufunguliwa rasmi
Watalii wakitazama vitu vinavyooneshwa katika Jumba la Makumbusho Kuu la Misri mjini Giza, Misri, Oktoba 14, 2025. (Xinhua/Ahmed Gomaa)

CAIRO - Jumba la Makumbusho Kuu la Misri (GEM) limefungwa kwa muda kwa umma kuanzia leo Jumatano Oktoba 15 hadi Novemba 3 kwa ajili ya ufunguzi wake rasmi, uliopangwa kufanyika mapema Novemba, kwa mujibu wa tangazo lililochapishwa Jumatatu wiki hii kwenye tovuti rasmi ya jumba hilo la makumbusho.

Baada ya kufunguliwa kwa karibu mwaka mmoja, jumba hilo la makumbusho litazinduliwa rasmi katika hafla kubwa Novemba Mosi na litafunguliwa tena kwa umma Novemba 4.

Kipindi cha majaribio cha kufungulikwa kwa jumba hilo la makumbusho kilijumuisha kumbi 12 zinazoonyesha maelfu ya kazi za sanaa za asili, vilevile Eneo Kuu linaloonyesha sanamu kinara za kihistoria na kazi za sanaa za asili kutoka vipindi tofauti vya historia ya kale ya Misri.

Katika kipindi chote cha kufunguliwa kwa baadhi ya sehemu, maafisa walikuwa wamefunga Ukumbi mkubwa wa Tutankhamun ili kuuhifadhi kama eneo kuu la ufunguzi huo mkubwa. Ukumbi huo utakuwa na mikusanyo yote ya mfalme huyu kijana – kazi za sanaa zipatazo 5,398 – zikiwemo za kinyago chake cha dhahabu, majeneza mawili, na hazina zingine, kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Misri, MENA.

Likiwa linapatikana karibu na piramidi mashuhuri za Giza na kuenea kwenye eneo lenye ukubwa wa mita za mraba karibu 500,000, Jumba la Makumbusho Kuu la Misri linatambulika kama jumba la makumbusho ya kiakiolojia kubwa zaidi duniani linaloonyesha ustaarabu mmoja, Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale ya Misri imesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha