IMF yahimiza nchi na maeneo ya Asia kuongeza mahitaji ya ndani, kuzidisha mafungamano ya kikanda

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 17, 2025

IMF yahimiza nchi na maeneo ya Asia kuongeza mahitaji ya ndani, kuzidisha mafungamano ya kikanda

Krishna Srinivasan (katikati), mkurugenzi wa Idara ya Asia na Pasifiki ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusu mtazamo wa uchumi wa Eneo la Asia na Pasifiki mjini Washington, D.C., Marekani, Oktoba 16, 2025. (Xinhua/Li Rui)

WASHINGTON - Huku zikikabiliwa na hatari kutoka kwenye mvutano wa kibiashara, nchi na maeneo ya Asia yanaweza kuongeza ukuaji kwa kuelekeza zaidi kwenye ukuaji unaotokana na mahitaji ya ndani na kuimarisha mafungamano ya kikanda, Krishna Srinivasan, mkurugenzi wa Idara ya Asia na Pasifiki ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) amesema jana Alhamisi kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusu mtazamo wa kiuchumi wa Eneo la Asia na Pasifiki mjini Washington.

"Hili ni eneo ambalo linategemea sana biashara ya nje. Kwa hiyo wakati wowote kunapokuwa na mishtuko kwenye biashara ya kimataifa, itaathiri Asia kiasi hicho zaidi,” Srinivasan amesema.

Akijibu swali kutoka Shirika la Habari la China, Xinhua, afisa huyo wa IMF amesema kuwa daima kuna "matokeo mazuri," licha ya hatari za kushuka zinazotokana na hali ya kutokuwa na uhakika katika biashara, udhaifu unaohusiana na madeni na mambo mengine.

"Asia ina fursa ya kuelekeza zaidi katika ukuaji unaoongozwa na mahitaji ya ndani," Srinivasan amesema, akiongeza kuwa mchango wa mahitaji ya ndani kwenye ukuaji katika eneo la Asia na Pasifiki umepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya janga la COVID-19.

Amesisitiza faida za mafungamano makubwa zaidi ndani ya kanda: Pato la Jumla linaweza kuongezeka kwa hadi asilimia 1.4 katika muda wa kati kwa Asia yote, na baadhi ya nchi ambazo zimefungua mlango zaidi na zimeunganishwa na minyororo ya kimataifa ya usambazaji bidhaa zitafaidika zaidi.

Kwa mujibu wa makadirio ya hivi karibuni ya IMF, ukuaji katika eneo la Asia-Pasifiki unatarajiwa kupungua kutoka asilimia 4.5 mwaka huu hadi asilimia 4.1 mwaka 2026.

“Licha ya ukuaji huo mdogo, kanda hiyo itaendelea kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji duniani, ikichangia asilimia takriban 60 mwaka huu na mwaka 2026,” Srinivasan amesema, akiongeza kuwa uhimilivu huo unaweza kuhusishwa na upakiaji wa mapema wa bidhaa za kuuzwa nje, maendeleo ya teknolojia, na sera jumuishi za uchumi mkuu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha