China yazindua mpango kuhimiza shoroba za kimataifa za usafirishaji wa kijani wa meli

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 20, 2025

Picha ikionyesha mwonekano wa Gati la Yangshan la Bandari ya Shanghai, mashariki mwa China, Desemba 18, 2024. (Xinhua/Fang Zhe)

Picha ikionyesha mwonekano wa Gati la Yangshan la Bandari ya Shanghai, mashariki mwa China, Desemba 18, 2024. (Xinhua/Fang Zhe)

SHANGHAI - Wizara ya Uchukuzi ya China imezindua Mpango wa Ushirikiano wa Kimataifa juu ya Ushoroba wa Usafirishaji wa Kijani wa Meli jana Jumapili kwenye Jukwaa la North Bund 2025 mjini Shanghai, ikitoa wito wa kufanya juhudi za pamoja za kujenga mfumo wa ikolojia wa usafirishaji wa meli ulio salama, wenye ufanisi na wa kijani zaidi duniani.

Mpango huo unajumisha hatua saba muhimu za kuhimiza ushirikiano wa kimataifa kwenye shoroba za usafirishaji wa kijani wa meli ambapo hatua hizo zinahusisha; kupanua shoroba za usafirishaji wa kijani wa meli kwa awamu tofauti, kuharakisha uundaji wa meli za kijani na zenye kutoa kaboni chache, kujenga bandari za kutotoa kaboni au kutoa kaboni karibu sifuri, kuongeza uwezo wa usambazaji wa mafuta wa kijani, kutumia kikamilifu ushirikiano kati ya soko na serikali, kunufaishana uzoefu bora, na kuunga mkono uvumbuzi.

Mafanikio kadhaa ya ushirikiano katika ujenzi wa shoroba za usafirishaji wa kijani wa meli yametangazwa katika baraza hilo, yakiwemo ya kuanzisha kwa pamoja ushoroba wa usafirishaji wa kijani wa meli kati ya Bandari ya Qingdao mashariki mwa China na Bandari ya Hamburg, Ujerumani.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, China imedumisha nafasi yake ya juu duniani katika muunganisho wa baharini kwa miaka kadhaa mfululizo, huku ikipanua hatua kwa hatua ufunguaji mlango na ushirikiano wa kimataifa katika sekta hiyo.

Wizara hiyo imesema, hadi kufikia Aprili mwaka huu, China ilikuwa imetia saini makubaliano ya baharini ya pande mbili au ya pande nyingi na nchi na maeneo 70.

Bandari kubwa kote China, zikiwemo Bandari za Shanghai na Bandari ya Ningbo-Zhoushan, zimeharakisha maendeleo ya miundombinu ya usambazaji wa kijani wa mafuta.

Jukwaa la North Bund 2025, ambalo ni la mara ya tano kufanyika, limeandaliwa kwa pamoja na Wizara ya Usafirishaji ya China na Serikali ya Mji wa Shanghai. Litaendelea hadi kesho Oktoba 21.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha