Kupamba moto kwa mapigano ya kijeshi Gaza kwasababisha vifo vya watu takriban 46 ingawa makubaliano ya kusimamisha mapigano yamesainiwa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 20, 2025

JERUSALEM/GAZA - Kupamba moto kwa mapigano ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza kati ya Israel na Hamas kumesababisha vifo vya watu 46 jana Jumapili, ingawa yamekuwa na makubaliano yanayoendelea ya kusimamisha mapigano, vyanzo vya habari ndani ya Israeli na Palestina vimesema.

Jeshi la Israel limesema katika taarifa yake kwamba askari wake wawili wameuawa katika shambulizi la Hamas mapema siku hiyo asubuhi. Wakati wa tukio hilo, Hamas ilirusha kombora la kupambana na vifaru na kufyatulia risasi wanajeshi wa Israel waliokuwa wakibomoa miundombinu mjini Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema.

Katika kujibu shambulizi hilo lililoripotiwa, IDF ilianzisha upigaji mabomu mfululizo kutoka angani na kupiga mizinga dhidi ya maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza.

Mamlaka za afya za Gaza zimesema Wapalestina 44 wameuawa katika mashambulizi hayo ya Israel.

Mahmoud Basal, msemaji wa Shirika la Ulinzi wa Raia la Gaza, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba wafanyakazi wa uwanja wa vita waliitikia miito zaidi ya 20 ya watu wanaohitaji msaada tangu asubuhi.

Baadaye Jumapili jioni, jeshi la Israel lilitangaza kuwa limeanza tena utekelezaji wa makubaliano ya kusimamisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Msemaji wa jeshi la Israel Avichay Adraee alisema katika taarifa yake kuwa "Vikosi vya Ulinzi vya Israel vimeanza kutekeleza tena makubaliano ya kusimamisha mapigano kulingana na maagizo kutoka ngazi ya kisiasa, baada ya kupiga mabomu mfululizo kutoka angani kwa kujibu ukiukaji wa makubaliano wa Hamas."

Makubaliano hayo ya kusimamisha mapigano, yaliyosimamiwa kwa upatanishaji wa Misri, Qatar, na Uturuki chini ya usimamizi wa Marekani, yamekuwa yakitekelezwa kuanzia Oktoba 10.

Chini ya makubaliano hayo, pande zote mbili ziliazimia kusitisha mapigano, kubadilishana wafungwa na mateka, kuondoka kwa vikosi vya Israel kutoka baadhi ya maeneo ya ukanda huo, na kuingia kwa msaada wa ubinadamu na mafuta ili kuruhusu timu za matibabu na msaada kuanza tena shughuli zao.

Hata hivyo, licha ya ahadi hizo, Israel na Hamas zote zimekuwa zikishutumiana kukiuka makubaliano ya kusimamisha mapigano.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha