WHO yasema DRC inaweza kutangaza kumalizika kwa mlipuko wa Ebola ifikapo Desemba

(CRI Online) Oktoba 20, 2025

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa mamlaka za afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zinaweza kutangaza kumalizika kwa mlipuko wa sasa wa Ebola mapema Desemba kama hakutakuwa na mgonjwa mpya aliyegunduliwa kabla ya wakati huo.

Tangazo hilo limetolewa jana Jumapili kwenye taarifa ya Ofisi ya WHO Kanda ya Afrika baada ya mgonjwa wa mwisho wa Ebola kuruhusiwa kutoka katika kituo cha matibabu kufuatia kupona kabisa, hatua ambayo ni muhimu katika vita dhidi ya virusi hatari vya ugonjwa huo nchini humo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa kupona kwa mgonjwa huyo kunaashiria mwanzo wa kuhesabu siku 42, na baada ya hapo mlipuko unaweza kutangazwa rasmi kuwa umemalizika, endapo hakutakuwa na mgonjwa mpya aliyebainika.

Mohamed Janabi, mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, amepongeza hatua iliyopigwa hadi sasa, akisema kuwa kupona kwa mgonjwa huyo wa mwisho, wiki sita tu baada ya mlipuko kutangazwa, ni mafanikio ya kushangaza.

Amesisitiza kuwa hali hiyo inaonesha nguvu ya ushirikiano, utaalamu wa kitaifa, na dhamira ya pamoja ya kushinda changamoto na kuokoa maisha.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha