China yachangia dola milioni 3.5 kwa ajili ya mpango wa msaada wa chakula nchini Zambia

(CRI Online) Oktoba 21, 2025

Hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Msaada wa Chakula wa Zambia, unaofadhiliwa na China kupitia Mfuko wa Maendeleo Duniani na Ushirikiano wa Kusini-Kusini kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), imefanyika jana Jumatatu mjini Lusaka, nchini Zambia.

Chini ya mradi huo, China imechangia dola za Marekani milioni 3.5 ili kuisaidia Zambia kununua tani takriban 5,641 za mahindi ndani ya nchi. Mahindi hayo yatasambazwa kwa muda wa miezi mitatu kwa wanufaika 188,057, ama kaya karibu 37,000, katika wilaya zilizoathiriwa zaidi na ukame za Majimbo ya Kusini na Magharibi.

Hafla ya makabidhiano ilihudhuriwa na Balozi wa China nchini Zambia Han Jing, Makamu Rais wa Zambia Mutale Nalumango, maafisa wa ubalozi na wawakilishi wengine wa serikali, sambamba na maafisa wa Kituo cha Kimataifa cha China kwa Mabadilishano ya Kiuchumi na Kiufundi (CICETE) na WFP, ambao ni washirika watekelezaji wa mpango huo.

Katika hotuba yake, Han amesema China itaendelea kuhamasisha rasilimali kupitia njia mbalimbali ili kuunga mkono maendeleo ya Zambia, akitolea mfano misaada mbalimbali iliyotolewa kwa wakati katika miaka ya hivi karibuni.

Naye Nalumango ameishukuru China kwa uungaji mkono wa China uliokuwa wa wakati na wenye kufaa, akibainisha kwamba misaada hiyo ya mara kwa mara katika sekta mbalimbali inaonesha uhusiano mzuri na wa kirafiki kati ya nchi hizo mbili.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha