Lugha Nyingine
Njia mpya ya usafirishaji kwenye bahari yachochea ukuaji wa asilimia zaidi ya 50 katika biashara ya Mji wa Shanghai na Nchi ya Peru

Zana na Vifaa vya teknolojia za kisasa vikinyanyua makontena katika Bandari ya Chancay, Peru, tarehe 14 Novemba 2024. (Xinhua/Li Mengxin)
SHANGHAI – Takwimu zilizotolewa jana na Idara ya Forodha ya Shanghai zimeonesha kuwa, njia ya usafirishaji wa meli ya "Chancay-Shanghai" imesafirisha shehena za bidhaa za tani 154,000 za kuagizwa na kuuzwa nje zenye thamani ya Yuan bilioni 3.97 (dola za Kimarekani karibu milioni 559.37) katika robo tatu za kwanza za mwaka huu, ikichochea ongezeko kubwa la asilimia 56.9 kuliko ile ya kipindi kama hicho cha mwaka uliopita katika Biashara ya mji wa Shanghai wa China na nchi ya Peru kufikia yuan bilioni 13.42.
Forodha hiyo imesema kuwa, ikilinganishwa na nusu ya kwanza ya mwaka 2025, wakati njia hiyo iliposafirisha bidhaa za tani 78,000 zenye thamani ya yuan bilioni 1.72, takwimu hizo mpya zinaonyesha ukuaji wa kasi, ikiimarisha njia hiyo kuwa "daraja jipya" la biashara kati ya China na Peru.
Imesema kuwa, hivi karibuni, shehena ya kwanza ya vitu vya kuoneshwa kwenye Maonyesho ya 8 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China yajayo iliwasili katika Bandari ya Yangshan ya Shanghai, ikiwa imesafirishwa kutoka Bandari ya Chancay ya Peru.
Shehena hiyo inajumuisha vitu 764, kama vile midori ya alpaca na vyombo vya ufundi wa ufinyanzi. Hasa, hii inamaanisha kuwa mara ya kwanza kwa bidhaa za maonyesho kusafirishwa kupitia njia hiyo ya usafirishaji wa meli tangu kuzinduliwa kwa ushoroba mpya wa nchi kavu na bahari katika Bahari ya Pasifiki, ambao unaunganisha Latini Amerika na Asia, mwishoni mwa 2024.
Bandari hiyo ya Chancay, ambayo ni kituo cha kina kirefu cha maji na bandari ya kwanza ya teknolojia za kisasa na ya kijani ya Amerika Kusini, ni mradi kinara wa ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja kati ya China na Peru, ambao umefupisha muda wa usafirishaji baharini kati ya nchi hizo mbili kutoka zaidi ya mwezi hadi siku karibu 23, wakati huohuo ikipunguza gharama za usafirishaji wa meli kwa asilimia angalau 20.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



