Pato la Taifa la China laongezeka kwa asilimia 5.2 katika robo tatu za kwanza

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 21, 2025

Wateja wakinunua bidhaa kwenye supamaketi mjini Zaozhuang, Mkoani Shandong, mashariki mwa China, Oktoba 15, 2025. (Picha na Sun Zhongzhe/Xinhua)

Wateja wakinunua bidhaa kwenye supamaketi mjini Zaozhuang, Mkoani Shandong, mashariki mwa China, Oktoba 15, 2025. (Picha na Sun Zhongzhe/Xinhua)

BEIJING - Pato la taifa la China (GDP) limeongezeka kwa asilimia 5.2 katika robo tatu za kwanza za mwaka 2025 likilinganishwa na mwaka jana wakati kama huo, takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya China (NBS) zimeonyesha jana Jumatatu ambapo GDP ya China imefikia yuan zaidi ya trilioni 101.5 (dola za Kimarekani karibu trilioni 14.3) katika robo tatu za kwanza.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa, katika robo ya tatu, Pato la Taifa liliongezeka kwa asilimia 4.8 likilinganishwa na mwaka jana kipindi kama hicho.

Zinaonyesha kuwa, katika ongezeko hilo, sekta ya huduma ilipanuka kwa asilimia 5.4 katika robo tatu za kwanza, ikipita ongezeko la asilimia 3.8 la sekta ya kuzalisha malighafi na ongezeko la asilimia 4.9 la sekta ya kuzalisha bidhaa.

"Kwa msingi wa kila robo ya mwaka, uchumi wa China uliongezeka kwa asilimia 1.1 katika robo ya tatu," NBS imesema.

"Tangu mwanzo wa mwaka huu, maendeleo ya uchumi wa China yamestahimili shinikizo na kupata upigaji hatua mkubwa uliopatikana kwa juhudi," amesema msemaji wa NBS, akiongeza kuwa shughuli za kiuchumi zimedumisha ufanisi tulivu kwa ujumla na ukuaji wa kasi.

Amesema, katika kipindi cha miezi tisa ya kwanza ya mwaka huu, pato la viwanda la China lililoongezwa thamani liliongezeka kwa asilimia 6.2 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana, na katika mwezi Septemba, pato hilo liliongezeka kwa asilimia 6.5, huku sekta za viwanda na madini zikirekodi ukuaji wa haraka.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, pato la huduma iliyoongezwa thamani la China lilipanda hadi yuan karibu trilioni 59.3 katika robo tatu za kwanza, likichukua asilimia 58.4 ya Pato la Taifa, ongezeko la asilimia 0.8 kuliko mwaka jana.

Takwimu zaidi zinaonyesha kuwa mauzo ya rejareja ya bidhaa za matumizi ya China yalipanda kwa asilimia 4.5 kufikia yuan karibu trilioni 36.59 katika robo tatu za kwanza. Mwezi Septemba, mauzo hayo ya rejareja ya bidhaa za matumizi yaliongezeka kwa asilimia 3 na kufikia yuan trilioni 4.2.

"Pato la kila mtu baada ya makato mbalimbali lilifikia yuan 32,509 katika kipindi cha Januari-Septemba, ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.2 baada ya kupunguza viwango vya bei" takwimu hizo zinaonesha.

Aidha, takwimu zinaonyesha kuwa, kiwango cha ukosefu wa ajira mijini kilichofanyiwa utafiti kwa wastani nchini China kilifikia asilimia 5.2 katika robo tatu za kwanza, ambapo kiwango hicho kilishuka kwa asilimia 0.1 kutoka Agosti hadi asilimia 5.2 mwezi Septemba.

Kwa mujibu wa takwimu hizo za NBS, uwekezaji wa mali zisizohamishika wa China ulipungua kwa asilimia 0.5 na kufikia yuan takriban trilioni 37.2 katika robo tatu za kwanza.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha