Vito vya thamani vyaibiwa kwenye Jumba la Makumbusho la Louvre mjini Paris, Ufaransa

(CRI Online) Oktoba 21, 2025

Mamlaka za Ufaransa zimesema Jumba la Makumbusho la Louvre mjini Paris lilifungwa kwa umma siku ya Jumapili "kwa sababu maalum" kufuatia uporaji ambapo vito tisa vyenye thamani kubwa ya kihistoria vimeibiwa ingawa hata hivyo hakukuwa na majeruhi walioripotiwa.

Kwa mujibu wa ripoti za awali, genge la wahalifu wanne waliojifunika nyuso wanadaiwa kuwa waliingia kwenye Ukumbi wa Sanaa wa Apollo wa jumba hilo la makumbusho kwa kuvunja madirisha yake, baada ya kupanda juu ya jumba hilo kwa kutumia lifti ya mizigo.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa Laurent Nunez, ambaye alitembelea eneo la tukio, ameyaelezea mabaki ya kihistoria yaliyoibiwa kuwa ni yenye thamani ya urithi "isiyoweza kukadiriwa". Amesema, jumba hilo la Makumbusho ya Louvre na Wizara ya Utamaduni wanatayarisha orodha ya vitu vilivyoibiwa na kutathmini thamani zao.

Ameeleza kuwa, wachunguzi kutoka makao makuu ya polisi ya Paris wamelinda eneo hilo na kuanza uchunguzi.

Vyombo vya habari vya Ufaransa vimeripoti kuwa miongoni mwa vitu hivyo vilivyoibiwa ni mkufu wa yakuti ambao ni moja kati ya vito vya Malkia Marie Amelie na Malkia Hortense, na tiara kutoka kwa Empress Eugenie.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha