Lugha Nyingine
Benki Kuu ya China yaeneza matumizi ya kimataifa ya RMB katika shughuli maalum iliyofanyika London, Uingereza

Picha iliyopigwa Oktoba 20, 2025 ikionyesha mwonekano wa shughuli maalum iliyoandaliwa na Benki Kuu ya China mjini London, Uingereza. (Xinhua/Li Ying)
LONDON - Benki Kuu ya China jana Jumatatu iliandaa shughuli maalum mjini London, Uingereza kueneza matumizi ya kimataifa ya renminbi (RMB), huku maafisa, wafadhili na watunga sera kutoka China na Uingereza wakitafuta njia mpya za kuzidisha ushirikiano wa mambo ya fedha ya kuvuka mipaka.
Wawakilishi takriban 100 kutoka Benki Kuu ya China, serikali ya Uingereza, Jiji la London, taasisi za fedha za kimataifa na taasisi za washauri bingwa walishiriki kwenye shughuli hiyo, ambayo ni sehemu ya Mfululizo wa Uenezaji wa RMB Kimataifa wa Benki hiyo Mwaka 2025. Majadiliano kwenye shughuli hiyo yalijikita katika kupanua nafasi ya RMB katika biashara ya kimataifa, uwekezaji na masoko ya fedha.
Jenny Young, naibu mkurugenzi wa biashara na masoko yanayoibukia katika Wizara ya Fedha ya Uingereza, amesema London sasa ina taasisi zaidi ya 40 za kifedha za China na kwamba Uingereza inathamini ushirikiano wake wa karibu na Benki Kuu ya China na benki nyingine za China zinazofanya kazi katika mji huo.
"Wakati China inaendelea kuchukua jukumu muhimu katika uchumi duniani, maendeleo ya bidhaa zenye uhusiano na RMB yanatoa fursa halisi," Young amesema.
James Michael Douglas Thomson, naibu mwenyekiti wa sera na rasilimali katika Shirika la Jiji la London, amesema nguvu ya mambo ya kifedha ya London na ushawishi wa kiuchumi wa China vinazidi kuunganishwa.
Akiwa amewahi kufanya kazi katika sekta ya huduma za mambo ya kifedha mwenyewe, Thomson amesema ameshuhudia kwa macho yake namna China imekuwa muhimu katika majadiliano kuhusu biashara duniani.
Tangu iliposaidia kuzindua soko la ng'ambo la RMB la London mwaka 2011, Benki Kuu ya China tawi la London imekuwa ikibeba jukumu ongozi katika kuendeleza utoaji wa huduma za uidhinishali, malipo na dhamana za RMB.
Kwa kutumia nafasi ya London kama lango linalounganisha Ulaya, Afrika na Mashariki ya Kati, tawi hilo linaendelea kuwa miongoni mwa taasisi za juu za China katika utoaji wa dhamana za ng’ambo kwenye maeneo hayo.

James Michael Douglas Thomson, naibu mwenyekiti wa sera na rasilimali katika Shirika la Jiji la London, akitoa hotuba kwenye shughuli maalum iliyoandaliwa na Benki Kuu ya China mjini London, Uingereza, Oktoba 20, 2025. (Xinhua/Li Ying)

Jenny Young, naibu mkurugenzi wa biashara na masoko yanayoibukia katika Wizara ya Fedha ya Uingereza, akitoa hotuba kwenye shughuli maalum iliyoandaliwa na Benki Kuu ya China mjini London, Uingereza, Oktoba 20, 2025. (Xinhua/Li Ying)

Picha iliyopigwa Oktoba 20, 2025 ikionyesha mwonekano wa shughuli maalum iliyoandaliwa na Benki Kuu ya China mjini London, Uingereza. (Xinhua/Li Ying)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



