Lugha Nyingine
China yasema vizuizi vya viza vya Marekani havitasitisha uhusiano kati ya China na nchi za Amerika ya Kati
BEIJING - Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Guo Jiakun amesema kutumia viza kama silaha hakutaziogopesha nchi makini, wala hakutasitisha uhusiano unaostawi kati ya China na nchi za Amerika ya Kati.
Guo ametoa kauli hiyo kwenye mkutano na waandishi wa habari jana Jumanne alipoulizwa kutoa maoni yake kuhusu tangazo la Marekani la kuweka vizuizi vya viza kwa raia wa nchi za Amerika ya Kati vilevile watu wa karibu wa familia zao ambao wanashirikiana na Chama cha Kikomunisti cha China na "kudhoofisha utawala wa kisheria katika Amerika ya Kati."
Akisema kuwa China imewasilisha malalamiko kwa Marekani kuhusu vizuizi hivyo vya viza, Guo amesema Marekani, kwa kisingizio cha "utawala wa kisheria," inatekeleza hatua zisizo halali kwa kuweka vikwazo vya upande mmoja ili kuzikandamiza kisiasa na kuzishurutisha kiuchumi kwa nchi na watu binafsi.
“Kwa kuweka sheria za ndani juu ya sheria za kimataifa na wajibu wake, Marekani inahujumu haki na maslahi halali ya nchi nyingine, inakiuka sana kanuni za usawa wa mamlaka na kutoingilia masuala ya ndani, na kuvuruga kwa kiasi kikubwa utaratibu wa kimataifa,” Guo amesema.
Amesema uchokozi wa Marekani wa kunyooshea vidole mawasiliano na ushirikiano wa nchi za Amerika ya Kati na China hauna msingi kabisa na unaonyesha kikamilifu kutoheshimu nchi za Amerika ya Kati.
“Hii kwa mara nyingine tena inaonyesha jinsi Marekani ilivyozoea kuwafanyia ubabe wengine na pia inaonyesha kiburi na upendeleo wa kuegemea upande mmoja uliokita mizizi wa wanasiasa husika,” amesema Guo.
Guo ameongeza kuwa China siku zote itakuwa rafiki na mshirika mzuri wa nchi za Amerika ya Kati, na itashirikiana nazo kuhimiza maendeleo na ustawi, na kujenga kwa pamoja jumuiya ya China na Latin Amerika yenye mustakabali wa pamoja.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



