Familia takriban 350 zatembea kilomita 50 kutoroka mzingiro wa mapigano El Fasher nchini Sudan

(CRI Online) Oktoba 22, 2025

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema jana Jumanne kwamba familia takriban 350 zimetembea umbali wa kilomita karibu 50 kwa siku nne, ili kukimbia mji uliozingirwa na mapigano ya kivita wa El Fasher nchini Sudan, na kufika katika mji wa Tawila wakiwa katika hali mbaya.

Imeongeza kuwa wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee, na wale waliojeruhiwa njiani, siku ya Jumapili na Jumatatu waliungana na watu zaidi ya laki sita waliokimbia makazi yao kutoka El Fasher, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini, na maeneo ya jirani, ambao sasa wanaishi Tawila.

"Umoja wa Mataifa na washirika wake wa kibinadamu wametoa chakula, maji na huduma za msingi za matibabu kwa watu wapya wanaowasili, lakini mahitaji yanazidi kwa mbali rasilimali zilizopo" ofisi hiyo imesema.

Imeongeza kuwa, familia nyingi zilizokimbia makazi yao zinakosa mahali pa kuishi, chakula cha kutosha na maji salama, na kwamba OCHA inafanya uratibu na mamlaka, wafadhili na washirika kuhamasisha uwezo, rasilimali na uungaji mkono wa ziada.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha