SADC yazindua ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu wa Tanzania

(CRI Online) Oktoba 22, 2025

Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imezindua rasmi Ujumbe wake wa Waangalizi wa Uchaguzi (SEOM) jana Jumanne ili kufuatilia uchaguzi mkuu wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mkuu wa SEOM Richard Msowoya ambaye ni spika wa zamani wa Bunge la Malawi, anayemwakilisha Mwenyekiti wa chombo cha SADC kuhusu Siasa, Ulinzi na Ushirikiano wa Usalama na Rais wa Malawi Arthur Peter Mutharika, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuialika SADC kuangalia uchaguzi huo.

Msowoya amesema ujumbe wao wenye waangalizi 80 kutoka nchi 10 wanachama wa SADC, utasambazwa katika mikoa 27 kati ya 31 ya Tanzania ili kufuatilia kipindi cha kabla, wakati na baada ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na kampeni, upigaji kura na kuhesabu kura.

Akisisitiza dhamira ya SADC ya kuimarisha demokrasia katika kanda hiyo, Msowoya amehimiza wadau wote wa kisiasa kuzingatia amani na kuheshimu utawala wa sheria wakati wa uchaguzi.

Msowoya amesema SEOM itatoa taarifa yake ya awali Oktoba 31, ikijumuisha kile walichokiona kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa Tanzania.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha