Lugha Nyingine
Rwanda yawa mwenyeji wa kongamano la kimataifa kuhimiza ushirikiano zaidi katika kilimo mseto
Wajumbe wa Kongamano la sita la Dunia kuhusu Kilimo Mseto (Agroforestry) ambalo limefanyika nchini Rwanda, wametoa wito wa ushirikiano thabiti ili kuharakisha upanuzi wa kilimo mseto duniani.
Kongamano hilo lililoanza kufanyika Jumatatu wiki hii na limepangwa kuendelea hadi Ijumaa mjini Kigali, limevutia washiriki zaidi ya 700 kutoka kote duniani, wakiwemo wakulima, watafiti, watunga sera, viongozi wa sekta binafsi, mashirika ya kiraia na wawakilishi wa vijana.
Akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa kongamano hilo siku ya hiyo Jumatatu, Rais wa Muungano wa Kimataifa wa Kilimo Mseto Patrick Worms, amesema kufanyika tena kwa kongamano hilo barani Afrika kunabeba umuhimu wa kiishara na kiutendaji, akisisitiza kuwa kilimo mseto kama sayansi ya kisasa kilizaliwa barani Afrika, na sasa kongamano hilo limerejea tena nyumbani.
Likifanyika chini ya kaulimbiu ya "Kilimo Mseto kwa Watu, Sayari, na Faida," kongamano hilo linatumika kama jukwaa la kubadilishana maarifa na uvumbuzi unaoboresha kilimo endelevu, uhimilivu wa tabianchi na ukuaji wa uchumi jumuishi.
Pia linalenga kuimarisha ushirikiano kati ya watafiti, serikali, sekta binafsi, na jamii za wakulima ili kujumuisha kilimo mseto katika ajenda za maendeleo za kitaifa na kimataifa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



