Daraja lilojengwa na China lafikia muunganisho kamili wa kimuundo nchini Tanzania

(CRI Online) Oktoba 23, 2025

Boriti ya mwisho ya Daraja la Mto Malagarasi, ambalo ni moja ya madaraja marefu zaidi ya reli nchini Tanzania, imefungwa kwa mafanikio, ikiashiria hatua kubwa katika mradi wa reli ya kati ya SGR.

Likijengwa na Shirika la Uhandisi wa Ujenzi la China (CCECC), daraja hilo lenye urefu wa mita 433.5 linatumika kama kiungo muhimu katika sehemu ya sita ya SGR, likiunganisha mikoa ya mashariki na magharibi mwa Tanzania.

Shirika hilo limesema katika taarifa yake kuwa jumla ya boriti 68 zimefungwa katika mazingira magumu, ambayo ni pamoja na mafuriko ya mara kwa mara na hali tata ya kijiolojia.

Limeongeza kuwa mbinu za hali ya juu za ujenzi na viwango vikali vya usalama vilihakikisha kutokuwepo kwa ajali na kutokuwepo kwa mkengeuko wakati wote wa ujenzi. Mara baada ya kuanza kufanya kazi, daraja hilo linatarajiwa kupunguza gharama za usafirishaji, kuongeza uwezo wa mizigo, na kuchochea ukuaji wa viwanda na biashara kando ya njia hiyo.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha