Lugha Nyingine
ICJ yatoa uamuzi kuwa Israel ina wajibu wa kuruhusu upitishaji wa msaada kwenda Gaza

Picha hii iliyopigwa Machi 12, 2025, ikionyesha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) mjini The Hague, Uholanzi. (Xinhua/Peng Ziyang)
THE HAGUE - Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imethibitisha tena jana Jumatano kwamba Israel ina wajibu wa kuwezesha uwasilishaji wa msaada wa ubinadamu katika Ukanda wa Gaza, ikiwa ni pamoja na msaada unaotolewa na mashirika ya Umoja wa Mataifa.
Israel ikiwa nchi inayokalia eneo, inatakiwa kutimiza wajibu wake chini ya sheria za ubinadamu za kimataifa,"mahakama hiyo imesema katika maoni yake ya ushauri usiolazimisha kisheria yaliyoombwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).
Mahakama hiyo imesema kuwa Israel "iko chini ya wajibu wa kukubaliana na kuwezesha mpango wa utoaji msaada chini ya Kifungu cha 59 cha Mkataba wa Nne wa Geneva," kwa kuwa wakazi wa Gaza "bado hawajapata msaada wa kutosha."
Majaji hao wameihimiza Israel "kuhakikisha kwamba wakazi wa eneo la Palestina linalokaliwa wana mahitaji muhimu ya maisha ya kila siku, ikiwemo chakula, maji, mavazi, matandiko ya vitanda, malazi, mafuta, vifaa tiba na huduma."
"Nchi inayokalia eneo hairuhusiwi kutumia sababu za usalama kwa kusitisha shughuli zote za msaada wa ubinadamu katika eneo linalokaliwa," mahakama hiyo imesema.
Israel ina wajibu "wa kuwezesha kwa kila namna iliyo ndani ya uwezo wake kuhimiza utekelezaji wa mpango wa utoaji msaada, ambao ni pamoja na msaada uliotolewa na Umoja wa Mataifa na vyombo vyake, hasa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utoaji Msaada na Miradi kuhusu Wakimbizi wa Palestina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA), mashirika mengine ya kimataifa na nchi za upande wa tatu, na kutozuia misaada hiyo."
Mahakama hiyo pia imesema kwamba Israel lazima "iheshimu na kulinda wafanyakazi na miundombinu yote ya misaada na matibabu," na kupiga marufuku "kuchukulia hali ya njaa ya raia kuwa mbinu ya vita."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



