Tamasha la muziki la Belgrade lasherehekea maadhimisho ya miaka 70 ya uhusiano kati ya China na Serbia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 23, 2025

BELGRADE - Tamasha la muziki la kuadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa urafiki kati ya China na Serbia limefanyika Jumanne jioni wiki hii kwenye Ukumbi wa kihistoria wa Matamasha wa Kolarac mjini Belgrade, Serbia.

Wasanii kutoka China na Serbia waliwasilisha programu iliyojumuisha pamoja mashairi bora ya Kichina na opera ya Ulaya. Watazamaji kutoka kote China na Serbia waliitikia kwa nderemo za shangwe wakati wote wa maonyesho.

Waziri wa Utamaduni wa Serbia Nikola Selakovic amesema tamasha hilo ni "moja ya mambo muhimu katika mwaka tunaposherehekea maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa urafiki kati ya watu wa Serbia na China - urafiki uliojengwa juu ya kuheshimiana, kuaminiana na kushirikiana."

Amesisitiza kwamba utamaduni "unawakilisha mwelekeo muhimu wa uhusiano wa pande mbili" na kusisitiza tena dhamira ya Serbia ya "kujenga mustakabali wa siku za baadaye pamoja" kupitia mawasiliano ya kitamaduni.

Kwa upande wake Balozi wa China nchini Serbia Li Ming amelielezea tamasha hilo kuwa ni kumbukumbu yenye mguso wa moyo kwa urafiki wa kina ulioanzishwa kwa zaidi ya miongo saba iliyopita, akisema kuwa tukio hilo linaonyesha kuongezeka kwa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, ambao umefikia ngazi mpya ambayo haijawahi kufikiwa kabla.

Tamasha hilo limeandaliwa kwa pamoja na Wizara ya Utamaduni na Utalii ya China, Ubalozi wa China nchini Serbia, na Wizara ya Utamaduni ya Serbia.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha