

Lugha Nyingine
China yasema kuimarisha ushirikiano kati ya China na ASEAN kunaingiza utulivu na uhakika kwenye maendeleo ya dunia
BEIJING - China na nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Asia Kusini Mashariki (ASEAN) ni majirani wa karibu wenye falsafa inayofanana ya maendeleo na maslahi yaliyoingiliana sana, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Guo Jiakun amesema jana Jumatano, akisisitiza kwamba ushirikiano huo wa kimkakati wa pande zote unaendelea kuimarishwa, ukiingiza utulivu na uhakika katika maendeleo ya Asia na dunia.
Guo ameyasema hayo alipoulizwa kutoa maoni yake kuhusu ushirikiano kati ya China na ASEAN kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Takwimu mpya zinaonyesha kuwa, katika robo tatu za kwanza za mwaka huu, thamani ya jumla ya biashara ya China ya uagizaji na uuzaji bidhaa nje na ASEAN ni yuan trilioni 5.57 (dola za kimarekani karibu bilioni 785), ongezeko la asilimia 9.6 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana. Katika kipindi hicho, ASEAN iliendelea kuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa China, na matukio kama vile Maonyesho ya China-ASEAN yamefanyika kwa mafanikio. Wakati kukiwa na kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na uhakika kutoka nje, ushirikiano kati ya China na ASEAN umekabiliana na changamoto na kupata mafanikio mengi.
"Mawasiliano ya ngazi ya juu kati ya China na ASEAN yanaongezeka kuwa ya mara kwa mara, yakijenga hali ya kuaminiana kisiasa kwa kina zaidi na kuimarisha msukumo wa maendeleo jumuishi," Guo amesema, akiongeza kuwa, pande zote mbili zinaweka umuhimu mkubwa sana kufungamana mikakati ya maendeleo na zimeunda Mpango Kazi wa Kutekeleza Ushirikiano wa Kimkakati wa Pande zote kati ya ASEAN na China (2026-2030).
Amesema, huku zikitumia kikamilifu faida zao bora zinazoendana pamoja, China na ASEAN zinaimarisha mafungamano na uhimilivu wa minyororo ya viwanda na usambazaji bidhaa.
"Ndani ya mwaka huu, pande hizo mbili zitatia saini rasmi Itifaki ya Uboreshaji wa Eneo la Biashara Huria 3.0 la China-ASEAN, ikiwezesha mafungamano ya kiuchumi ya kikanda na biashara duniani," amebainisha.
Guo amesema kuwa Reli ya China-Laos na Reli ya Mwendokasi ya Jakarta-Bandung zinafanya kazi kwa utulivu, zikiboresha zaidi mawasiliano na kuchochea ukuaji kwenye njia zao husika.
Ameongeza kuwa ushirikiano katika maeneo yanayoibuka kama vile akili mnemba na uchumi wa kidijitali unastawi, hali ambayo imesaidia kujenga matarajio mapya kwa maendeleo yanayochochewa na uvumbuzi.
Guo pia ameeleza kuwa mawasiliano ya kitamaduni kati ya China na ASEAN yanaongezeka kwa kasi na kwamba Mwaka wa Mawasiliano ya Watu kati ya China na ASEAN umezaa matunda katika elimu, vijana, taasisi za washauri bingwa na ushirikiano wa vyombo vya habari.
"China itashirikiana na nchi za kikanda kujenga maskani ya pamoja yenye amani, usalama na ulinzi, ustawi, kupendeza na utulivu na kusukuma mbele ujenzi wa jumuiya iliyo karibu zaidi ya China na ASEAN yenye mustakabali wa pamoja," msemaji huyo amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma