Lugha Nyingine
China yapinga EU kuziorodhesha kampuni za China kwenye kifurushi cha vikwazo dhidi ya Russia
BEIJING - China inauhimiza Umoja wa Ulaya (EU) kuacha mara moja kuziorodhesha kampuni za China kwenye duru yake ya 19 ya vikwazo vya EU dhidi ya Russia, msemaji wa Wizara ya Biashara ya China amesema wakati akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari jana Alhamisi.
“Licha ya mazungumzo na juhudi za mara kwa mara za China za kupinga, EU imekataa kubadilisha mwelekeo, kwa mara nyingine tena ikiziorodhesha kampuni za China kwenye duru yake ya 19 ya vikwazo dhidi ya Russia, na kuweka vikwazo kwa viwanda vikubwa vya kusafisha mafuta na wafanyabiashara wa China kwa mara ya kwanza,” msemaji huyo amesema, akielezea malalamiko makali na upingaji mkali wa China kwa hatua hizo.
Msemaji huyo amesema kuwa China imekuwa ikipinga kithabiti vikwazo vya upande mmoja visivyo na msingi wa sheria za kimataifa au visivyopata idhini ya Umoja wa Mataifa.
Amefafanua kuwa, vitendo hivyo vya EU vimekwenda kinyume cha moyo wa maafikiano yaliyofikiwa kati ya viongozi wa China na EU, vimeharibu vibaya ushirikiano wa pande mbili katika sekta za uchumi na biashara, na kuathiri usalama wa nishati duniani.
Msemaji huyo amesema, "China inaihimiza EU kuacha mara moja kuziorodhesha kampuni za China kwenye vikwazo hivyo, na inaionya haitakwenda mbali zaidi katika njia potofu", akieleza kuwa, China itachukua hatua za lazima, na kulinda kithabiti haki na maslahi halali ya kampuni za China, pamoja na usalama wake wa nishati na maendeleo ya uchumi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



