Lugha Nyingine
Watu zaidi ya 120 wafariki katika mafuriko nchini Niger
Naibu msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amesema kuwa watu zaidi ya 120 wamefariki kutokana na mafuriko makubwa nchini Niger mwaka huu.
Haq amesema hayo jana Alhamisi kwenye mkutano wa kila siku na waandishi wa habari, akiongeza kuwa mafuriko wakati wa msimu wa mvua wa mwaka huu, ambao kwa kawaida huanza mwezi Juni, yameathiri watu wapatao 550,000, huku maeneo ya Dosso, Tillaberi na Maradi yakiathiriwa zaidi.
Akinukuu Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu, Haq amesema kuwa mafuriko hayo pia yameharibu nyumba karibu 55,000 huku ekari zaidi ya elfu kumi za mashamba zikiwa zimezama kwenye maji.
Amesema Umoja wa Mataifa na washirika wake wa kibinadamu wanafanya kazi kuunga mkono juhudi za misaada zinazoongozwa na serikali ya Niger, lakini rasilimali bado hazitoshelezi, huku mpango wa mwaka huu wa Niger wa kutoa misaada ya kibinadamu ukiwa na thamani ya dola za Kimarekani milioni 603, na chini ya asilimia 20 ndizo zimepatikana.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



