Tanzania na UNDP zaanzisha mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhifadhi bioanuwai

(CRI Online) Oktoba 24, 2025

Tanzania ikishirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Alhamisi walizindua mradi wenye thamani ya dola milioni 37.4 za kimarekani, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuhifadhi bioanuwai, na kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa.

Mradi huo umefadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) na kutekelezwa kupitia shirika la Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi huo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ya Tanzania Dkt. Hassan Abbasi amesema, awamu ya kwanza ya mradi huo itatekelezwa kwenye Msitu wa Chome katika Mkoa wa Kilimanjaro na hifadhi za Amani, Magamba, na Nilo katika Mkoa wa Tanga.

Amebainisha kuwa mradi huo unaonyesha imani ya jumuiya ya kimataifa juu ya sera za Tanzania kuhusu tabianchi na mazingira.

Naye Mkurugenzi wa mazingira katika ofisi ya makamu wa rais wa Tanzania Kemilembe Mutasa amesema mradi huo pia unaunga mkono mkakati wa taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambao unalenga kuhamasisha asilimia 80 ya kaya kutumia nishati safi kabla ya mwaka 2030.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha